Mbona hatuoni maiti akiadhibiwa pale kunapofukuliwa kaburi lake?

Swali: Kuhusu kufukua makaburi haya ambayo kwa mtazamo wako, kama alivyotaja Shaykh, baadhi yao hawakukuta chochote ndani yake na baadhi yao hawakukuta isipokuwa mfupa mdogo tu?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mwanadamu huteketea kila kitu chake isipokuwa kijifupa cha mgogo (عجب الذنب). Huo hubaki na kutokana nao uumbaji utarejeshwa siku ya Qiyaamah.”

Ni mfupa mdogo sana ambao uumbaji utaumbwa tena kutoka kwake siku ya Qiyaamah. Adhabu siyo maalum kwa mwili tu, bali sehemu yake kubwa iko juu ya roho na roho ina jambo kubwa sana. Ikiwa iko katika kumcha Allaah, basi ina neema ya Pepo, na ikiwa ni kinyume cha hivyo, basi ina adhabu yake ya Moto. Tunamuomba Allaah (Ta´ala) atulinde. Ni kama Alivyosema (Ta´ala) kuhusu watu wa Fir´awn:

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا

“Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni… ”

Kwa maana roho zao na miili yao:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“… na Siku itakayosimama Saa [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa!”[1]

Kwa hiyo roho zina sehemu yake ya adhabu – nayo ndiyo nyingi zaidi katika maisha ya ndani ya kaburi – na mwili pia una sehemu yake kadiri Allaah anavyotaka. Hali zao zinaweza kuwa namna hiyo. Huenda mwili pia ukapata sehemu yake, japokuwa watu hawahisi. Allaah amewaonyesha baadhi ya waja wake adhabu hii duniani kabla ya Aakhirah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona hilo. Allaah alimjulisha kuhusu makaburi mawili yaliyokuwa yanaadhibiwa kwa sababu ya kusengenya na kutokujisitiri na mkojo. Hayo yametokea duniani kabla ya Aakhirah.

Imethibiti kwetu kwa njia nyingi na ametaja hilo Ibn Rajab katika kitabu cha “Ahwaal-ul-Qubuur”, kuwa imesimuliwa kwa njia nyingi – kwa waliokuwepo na wasiokuwepo – na wanazuoni wameeleza visa vingi vikubwa kuhusu makaburi ambayo watu wake walionekana wakiwa katika adhabu. Miongoni mwa hayo ni kwamba wakati wa kuondoka baada ya mazishi, huenda baadhi yao akasahau kifaa chake kama jembe au kifaa kingine, kisha wakafungua kaburi ambapo wakalikuta linawaka moto juu ya mwenye kaburi. Tunamuomba Allaah hifadhi. Katika wakati huohuo wanaona kwa macho yao kaburi hilo likiwaka moto.

Kadhalika matukio mengine ambapo wanakuta kile kifaa walichokisahau, kama koleo, chuma au kitu kingine kinawaka moto juu ya mwenye kaburi. Kisha wanawauliza watu wa maiti hali yake ilikuwaje ambapo wanajibu kwamba alikuwa hivi na hivi; huyu alikuwa anapuuza swalah, huyu alikuwa na hali fulani na fulani. Hivyo adhabu iliharakishwa kwake tangu alipoingia kaburini.

Shaykh ´Abdullaah amewatajia mfano wa kile kinachotokea duniani ambacho kinaweza kulinganishwa na mambo ya makaburi, nayo ni usingizi: watu wawili wamelala pamoja, mmoja anaona ndoto yenye neema na faraja, na mwingine anaona ndoto yenye adhabu na mateso. Anapoamka, mmoja anafurahia na mwingine anaamka akiwa mchovu, koo lake limekauka, amezidiwa na dhiki, jasho na hali ngumu na hivyo akidhani ndoto ile ni kweli kutokana na alichokiona cha adhabu na maumivu. Mwingine anaona kuwa yuko katika raha, pamoja na marafiki, katika utulivu na faraja. Huyu anaamka akiwa amechoka na yule mwingine anaamka akiwa ametulia, ilihali wote wako karibu – mume na mke, mtoto na ndugu yake au watu wawili safarini – wote wako karibu katika hema au jangwani, hakuna baina yao isipokuwa umbali mdogo sana. Hata hivyo huyu yuko katika adhabu na huyu katika neema. Hivyo mambo ambayo Allaah (Ta´ala) ameyakadiria kwa waja siyo kama yale wanayoyajua watu na kuyahisi katika hali ya macho yao ya kawaida. Allaah mdiye Mwenye kutakwa msaada.

[1] 40:46

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3258/نعيم-البرزخ-وعذابه-على-الروح-والجسد-معا
  • Imechapishwa: 12/10/2026