Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amepwekeka na sifa maalum. Tutazungumzia zile zilizotajwa na mtunzi wa kitabu ikiwa ni pamoja na zifuatazo:

1 – Nabii wa mwisho. Amesema (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[1]

2 – Kiongozi wa Mitume. Dalili yake imekwishatangulia.

3 – Haitimii imani ya mja mpaka aamini Ujumbe wake. Amesema (Ta´ala):

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao… “

Mitume wengine hutumwa kwa watu maalum kila mmoja kwa watu wake.

4 – Watu hawatohukumiwa isipokuwa baada ya uombezi wake. Dalili ya hilo zimetangulia katika maudhui kuhusu uombezi.

5 – Ummah wake utazitangulia kuingia Peponi nyumati zingine. Hilo ni kutokana na kuenea kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sisi ni wa mwisho na wa mwanzo wenye kutangulia siku ya Qiyaamah.”[2]

Tayari imekwishatangulia.

6 – Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye atakayebeba bendera ya sifa siku ya Qiyaamah. Wenye kumsifu watakuwa chini yake. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ndiye mtukufu wa wana Aadam siku ya Qiyaamah na wala sijikharishi na itakuwa mkononi mwangu bendera ya himdi na wala sijifakharishi. Hakuna Mtume yeyote siku hiyo, kuanzia Aadam na wengineo, isipokuwa atakuwa chini ya bendera yangu. Mimi ndiye wa kwanza nitayefufuliwa na ardhi na wala sijifakharishi.”[3]

Ameipokea at-Tirmidhiy. Sehemu ya kwanza na ya mwisho imepokelewa na Muslim.

7 – Mwenye cheo kinachosifika. Kwa msemo mwingine yeye ndiye mwenye kitendo kitachomfanya kusifiwa na Muumba na viumbe. Amesema (Ta´ala):

عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا

”Hapana shaka Mola wako atakuinua cheo kinachosifika.”[4]

Cheo hichi ni miongoni mwa yale mambo yatayopatikana katika sifa zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Qiyaamah kukiwemo uombezi na mengineyo.

8 – Mwenye Hodhi itakayoendewa. Makusudio ni Hodhi kubwa itakayoendewa na watu wengi. Kuhusu Hodhi kama Hodhi imepokelewa kwamba kila Mtume anayo Hodhi.

09, 10, 11 – Kiongozi wa Mitume, muhubiri wao na mwenye uombezi wao. Ubayy bin Ka´b amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Itapokuwa siku ya Qiyaamah nitakuwa ni kiongozi wa Manabii na muhubiri wao na mwenye uombezi wao na wala sijifakharishi.”[5]

Ameipokea at-Tirmidhiy na amesema kuwa ni nzuri.

12 – Ummah wake ndio wa mwisho. Amesema (Ta´ala):

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ

“Mmekuwa Ummah bora uliotolewa kwa watu.”[6]

Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ َ

“Enyi wana wa Israaiyl! Ikumbukeni neema Yangu niliyokuneemesheni na hakika Mimi nimekufadhilisheni juu ya walimwengu wengineo.”[7]

Makusudio ni katika ulimwengu wa zama zao.

[1] 33:40

[2] Muslim (856, 22) na tamko lake liko kwa al-Bukhaariy (876).

[3] at-Tirmidhiy (3148, 3615) ambaye amesema:

”Ni nzuri na Swahiyh.”

Ameipokea vilevile Ibn Maajah (4308). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (1571). Muslim (2278, 03).

[4] 17:79

[5] Ahmad (05/137, 138) na at-Tirmidhiy (3615) ambaye amesema:

“Hadiyth ni nzuri.”

Ameipoeka vilevile Ibn Maajah (4314), al-Haakim (01/71) na (04/78) ambaye amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Takhriyj-ul-Mishkaah” (5768).

[6] 03:110

[7] 02:47

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 136-138
  • Imechapishwa: 12/12/2022