Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtu bora katika Ummah wake ni Abu Bakr asw-Swiddiyq, kisha ´Umar al-Faaruuq, kisha ´Uthmaan Dhuun-Nuurayn halafu ´Aliy al-Murtadhwaa (Radhiya Allaahu ´anhum). Kutokana na yale yaliyopokea ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Tulikuwa tukisema, ilihali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yuko hai: “Mbora wa Ummah huu baada ya Mitume wake ni Abu Bakr, kisha ´Umar kisha ´Uthmaan kisha ´Aliy.” Khabari hizo zinamfikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hazikatai.””[1]

Kumesihi mapokezi kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

“Mbora wa Ummah huu baada ya Mitume wake ni Abu Bakr, kisha ´Umar. Lau ningependa, ningemtaja wa tatu.”[2]

Abud-Dardaa amepokea kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Jua halijachomoza wala kuzama juu ya yeyote, baada ya Mitume na Manabii, kwa aliye bora kuliko Abu Bakr.”[3]

Yeye ndiye mwenye haki katika viumbe vya Allaah kwa uongozi baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na fadhilah zake, kutangulia kwake mbele na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumtanguliza aongoze swalah mbele ya Maswahabah wote (Radhiya Allaahu ´anhum). Maswahabah wote wameafikiana juu ya kumtanguliza mbele na kumpa mkono wa usikizi na utiifu –Allaah asingeacha wote wakaafikiana juu ya upotevu.

Baada yake kunakuja ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) kutokana na fadhilah zake na Abu Bakr kumpokeza. Kisha anafuata ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) kwa kuteuliwa na waliofanya mashauriano. Kisha anafuata ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kutokana na fadhilah zake na kuafikiana watu wa wakati wake. Hawa ndio makhaliyfah waongofu na wenye kuongoza ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yao:

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Ziumeni kwa magego.”[4]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Uongozi baada yangu utakuwa kwa miaka thelathini.”[5]

Khaliyfah wa mwisho alikuwa ni ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

MAELEZO

Swahabah ni yule ambaye alikusanyika na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kumuamini na akafa juu ya imani hiyo.

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Maswahabah wabora wa Mitume. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Bora ya watu ni wa karne yangu.”[6]

Hadiyth hii ameipokea al-Bukhaariy na wengine.

Maswahabah bora ni Muhaajiruun kwa sababu ya kukusanya kwao kati ya Hijrah na nusura. Kisha wanafuatia Answaar.

Bora ya Muhaajiruun ni wale makhaliyfah wanne waongofu; Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum).

[1] al-Bukhaariy (3655) na (3697).

[2] Ahmad (1/106/110) na Ibn Abiy ´Aasim (1201). al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni Swahiyh katika ”Takhriyj-us-Sunnah” (2/570).

[3] Ahmad katika ”Fadhwaa´il-us-Swahaabah” (135), Abu Nu´aym (3/325), Ibn Abiy ´Aasim (1224) na wengine.

[4] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidiy (2678), Ahmad (4/126-127), ad-Daarimiy (1/44-45), Ibn Maajah (42-43), al-Haakim (1/95) na wengine. Imaam Ibn Hibbaan, Imaam al-Ajjurriy na Imaam al-Albaaniy (Rahimahumu Allaah) wamesema kuwa ni Swahiyh. Tazama “Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (2/344) ya Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah).

[5] Abu Daawuud (4646), at-Tirmidhiy (2226), Ahmad (5/221), at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (6444), al-Hakiym (3/145) na wengineo.

[6] Abu Daawuud (4646, 4647), at-Tirmidhiy (2226) ambaye ameifanya kuwa nzuri. Ameipokea vilevile an-Nasaa´iy katika ”Fadhwaa´il-us-Swahaabah” (52), al-Haakim (03/71) na (145) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Aidha ameipokea Ahmad katika “al-Musnad” yake (05/220, 221) katika ”Fadhwaa´il-us-Swahaabah” (789, 790, 1027), Ibn Hibbaan (1534, 1535), Ibn Abiy ´Aaswim katika “as-Sunnah” (02/562), at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (13, 136, 6442), at-Twayaalisiy (1107) na al-Bayhaqiy katika “Dalaa-il-un-Nubuwwah” (06/34).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 138-141
  • Imechapishwa: 12/12/2022