Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Muhammad ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam), ndiye Nabii wa mwisho na ndiye kiongozi wa Mitume. Imani ya mja haisihi mpaka aamini Ujumbe wake na ashuhudie utume wake. Watu hawatofanyiwa hesabu siku ya Qiyaamah isipokuwa baada ya uombezi wake. Hakuna Ummah wowote utaoingia Peponi siku ya Qiyaamah isipokuwa baada ya kuingia kwanza Ummah wake. Yeye ndiye mwenye bendera ya sifa, Cheo kinachosifika na ndiye mwenye hodhi kubwa. Yeye ndiye kiongozi wa Mitume na ndiye muhubiri wao na ndiye mwenye uombezi wao. Ummah wake ndio Ummah bora kabisa na Maswahabah wake ndio wabora kuliko Maswahabah wa Mitume wengine (´alayhimus-Salaam).

MAELEZO

Viumbe bora mbele ya Allaah ni Mitume. Kisha wanafuatia Manabii. Kisha wanafuatia wale wakweli. Kisha wanafuatia mashahidi. Kisha wanafuatia waja wema. Allaah ametaja matabaka haya katika Kitabu Chake pale aliposema:

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[1]

Bora ya Mitume ni wale wakubwa katika wao. Nao ni watano; Nuuh, Ibraahiym, Muusa, ´Iysaa na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Allaah amewataja sehemu mbili katika Kitabu Chake. Katika “al-Ahzaab”:

وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ 

“Na wakati Tulipochukua kutoka kwa Manabii fungamano lao, na kutoka kwako na kutoka kwa Nuuh na Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa mwana wa Maryam.”[2]

Katika “ash-Shuuraa”:

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَى

“Amekuwekeeni Shari´ah katika dini yale aliyomuusia kwayo Nuuh, na ambayo tumekufunulia Wahy na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa.”[3]

Mbora wao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi ndiye bwana wa watu siku ya Qiyaamah.”[4]

Kuna maafikiano juu yake.

Kuswali kwao nyuma yake katika usiku wa Mi´raaj na dalili nyenginezo.

Kisha anayefuata ni Ibraahiym. Yeye ndiye baba wa Mitume na mila yake ndio msingi wa mila. Kisha anayefuata ni Muusa. Yeye ndiye mbora wa Mitume wa wana wa israaiyl na Shari´ah yake ndio msingi wa Shari´ah zao. Kisha anafuata Nuuh na ´Iysaa. Hakuna uhakika wa kufadhilisha kati yao. Kwa sababu kila mmoja katika wao ana sifa za kipekee.

[1] 04:69

[2] 33:07

[3] 42:13

[4] al-Bukhaariy (4712) na Muslim (327, 194).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 134-136
  • Imechapishwa: 12/12/2022