114. Njia tatu za kupatikana uongozi katika Uislamu

Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Sunnah ni kuwasikiliza na kuwatii viongozi na watawala wa waislamu na wa waumini. Ni mamoja wawe wema au waovu muda wa kuwa hawajaamrisha kumuasi Allaah, katika hali hiyo kutakuwa hakuna utiifu kwa yeyote katika kumuasi Allaah.

Yule ambaye atashika uongozi na watu wakakusanyika juu yake na kumridhia – au vilevile ikiwa atashika madaraka kwa nguvu mpaka akawa kiongozi, anakuwa ni kiongozi na huitwa “kiongozi wa waumini” na ni wajibu kumtii na ni haramu kupingana naye, kumfanyia uasi na kufarikisha umoja wa waislamu.

MAELEZO

Uongozi ni nafasi na jukumu kubwa. Maana yake ni kusimamia na kuongoza mambo ya waislamu kwa njia ya kwamba mtu huyo ndiye anakuwa muwajibikaji wa kwanza katika hayo. Ni faradhi yenye kutosheleza. Mambo ya watu hayawezi kusimama isipokuwa kwa jambo hilo.

Uongozi unapatikana kwa moja ya mambo matatu:

1 – Kuteuliwa na kiongozi mtangulizi. Hivo ndivo ilivyokuwa katika uongozi wa ´Umar bin al-Khattwaab. Aliteuliwa na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh).

2 – Kukubaliana kwa Ahl-ul-Hall wal-´Aqd. Ni mamoja ni watu maalum walioteuliwa na kiongozi aliyetangulia. Hivo ndivo ilivyokuwa katika uongozi wa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Ahl-ul-Hall wal-´Aqd walioteuliwa na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) walikubaliana kumchagua. Haijalishi kitu hata kama Ahl-ul-Hall wal-´Aqd hao hawakuteuliwa. Kwa mujibu wa maoni moja wapo hivo ndivo ilivokuwa katika uongozi wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh). Hivo vilevile ndivo ilivyokuwa katika uongozi wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

3 – Kwa nguvu na kimabavu. Hivo ndivo ilivyokuwa katika uongozi wa ´Abdul-Malik bin Marwaan wakati alipomuua Ibn-uz-Zubayr na uongozi ukatimia kwake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 17/12/2022