Kumtii khaliyfah na watawala wengine ni jambo la lazima katika mambo yasiyokuwa kumuasi Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kusikiliza na kutii kwa muislamu ni jambo la lazima katika anayoyapenda na kuyachukia muda wa kuwa hajaamrishwa maasi. Akiamrishwa maasi, basi hakuna kusikiliza wala kutii.”[2]

Kuna maafikiano juu yake.

Ni mamoja kiongozi huyo ni mwema, kwa msemo mwingine anatekeleza maamrisho ya Allaah hali ya kuyafanya na kuyaacha, au ni muovu ambaye anatenda madhambi makubwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Zindukeni! Yule ambaye atatawalishiwa mtawala na akaona anafanya kitu katika maasi, basi achukie yale anayoyaona katika kumuasi Allaah na asiondoe mkono kutoka katika utiifu.”[3]

Ameipokea Muslim.

Hajj na jihaad zinakuwa endelevu na zenye kutekelezwa pamoja na viongozi. Ni sawa kuswali nyuma yao swalah ya ijumaa. Ni mamoja ni wema au waovu. Kwa sababu kupingana nao katika hayo kunapelekea kufarikisha umoja na waislamu na kuwaasi.

[1] 04:59

[2] al-Bukhaariy (7144) na Muslim (1839, 38).

[3] Muslim (1855, 66).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 157
  • Imechapishwa: 17/12/2022