Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Tunashuhudia watu kumi kuwa Peponi kama walivyowashuhudilia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi aliposema:

“Abu Bakr yuko Peponi, ´Umar yuko Peponi, ´Uthmaan yuko Peponi, ´Aliy yuko Peponi, Twalhah yuko Peponi, az-Zubayr yuko Peponi, Sa´d yuko Peponi, Sa´iyd yuko Peponi, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf yuko Peponi na Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah yuko Peponi.”[1]

Vivyo hivyo kila yule ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimshuhudilia Pepo, na sisi pia tunamshuhudilia. Kama aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“al-Hasan na al-Husayn ni viongozi wa vijana wa Peponi.”[2]

Vilevile aliposema kumwambia Thaabit bin Qays:

“Kwa hakika ni mtu wa Peponi.”[3]

Hatumkatii muislamu yeyote Pepo wala Moto isipokuwa yule ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkatia. Lakini hata hivyo tunatarajia mema kwa mwema na tunakhofu kwa mtenda maovu.

MAELEZO

Kumshudilia mtu Pepo au Moto si jambo linalotokana na akili. Ni jambo linakuwa kwa mujibu wa dalili za Shari´ah. Yule ambaye dalili za Shari´ah zinamshudilia basi nasi tunamshuhudilia. Vinginevyo hatufanyi hivo. Lakini sisi tunataraji wema kwa mwema na tunachelea kwa mtenda maovu. Kumshudilia mtu Pepo na Moto kumegawanyika sampuli mbili:

1 – Kulikoenea.

2 – Maalum.

Ushuhuda ulioenea ni ule uliofungamana na sifa. Kwa mfano mtu akashuhudilia kuwa kila muumini yuko Pepo au kila kafiri yuko Motoni au mfano wa hivo miongoni mwa sifa ambazo Shari´ah imezifanya kuwa ni sababu ima ya kuingia Peponi au Motoni.

Ushuhuda maalum ni ule uliofungamana na mtu kwa dhati yake. Kwa mfano tukashuhudilia kuwa mtu maalum yuko Pepo au tukashuhudia mtu maalum kuwa yuko Motoni. Kwa hivyo hatumlengi yeyote isipokuwa yule aliyelengwa na Allaah au Mtume Wake.

[1] Abu Daawuud (4649) na (4650), at-Tirmidhiy (3748) na (3757), Ibn Maajah (134), Ahmad (1/187/189) na Ibn Abiy Aasim (1428), (1431) na (1436). al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni Swahiyh katika ”Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (4010).

[2] at-Tirmidhiy (3768) na Ahmad (3/166/167). Imaam at-Tirmidhiy (Rahimahu Allaah) amesema ”Hadiyth Hasan na Swahiyh.”

[3] al-Bukhaariy (3613) na Muslim (119).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 144-145
  • Imechapishwa: 14/12/2022