Watu waliolengwa kuwa wako Peponi ni wengi. Miongoni mwao ni wale kumi waliobashiriwa kuingia Peponi. Wamefanywa maalum kwa sifa hii kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewakusanya katika Hadiyth moja pale aliposema:

“Abu Bakr yuko Peponi, ´Umar yuko Peponi, ´Uthmaan yuko Peponi, ´Aliy yuko Peponi, Twalhah yuko Peponi, az-Zubayr yuko Peponi, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf yuko Peponi, Sa´d bin Abiy Waqqaas yuko Peponi, Sa´iyd bin Zayd yuko Peponi na Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah yuko Peponi.”[1]

Ameipokea at-Tirmidhiy na akaisahihisha al-Albaaniy.

Tumeshawazungumzia wale makhaliyfah wanne waongofu na kwamba waliosalia wamekusanywa katika shairi hili:

Sa´iyd, Sa´d, ´Awf na Twalhah

´Aamir na az-Zubayr mwenye kusifiwa

Twalhah ni mwana wa ´Ubaydullaah anayetokana na ukoo wa Taym bin Murrah. Ni mmoja katika wale watu nane waliotangulia katika Uislamu. Aliuliwa katika vita vya Jamal katika Jamaadaa al-Aakhirah mwaka wa 36 baada ya kuhajiri akiwa na miaka 64.

az-Zubayr ni mwana wa al-´Awaam anayetokana na ukoo wa Quswayy bin Kilaab mtoto wa shangazi yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliondoka siku ya Jamal kumuua ´Aliy njiani akakutana na Ibn Jarmuuz ambapo akamuua katika Jamaadaa al-Awwaal mwaka wa 36 baada ya kuhajiri akiwa na miaka 67.

´Abdur-Rahmaan bin ´Awf anayetokana na ukoo wa Zahrah bin Kilaab. Alifariki mwaka wa 32 baada ya kuhajiri na akazikwa al-Baqiy´.

Sa´d bin Abiy Waqqaas. Ni mwana wa Maalik anayetokana na ukoo wa ´Abd Manaaf bin Zahrah. Yeye ndiye wa kwanza aliyerusha mkuki katika njia ya Allaah.  Alifariki katika kasiri yake huko al-´Aqiyq maili kumi kutokea al-Madiynah na akazikwa al-Baqiy´ mwaka wa 55 baada ya kuhajiri akiwa na miaka 82.

Sa´iyd bin Zubayr. Ni mwana wa Zayd bin ´Amr bin Nufayl al-´Adawiy. Alikuwa ni miongoni mwa wale wa awali waliotangulia katika Uislamu. Alifariki al-´Aqiyq na akazikwa al-Madiynah mwaka wa 51 baada ya kuhajiri akiwa na miaka sabini na kitu.

Abu ´Ubaydah. Yeye ni ´Aamir mwana wa ´Abdullaah bin al-Jarraah anayetokana na ukoo wa Fihr. Ni miongoni mwa wale wa awali waliotangulia katika Uislamu. Alifariki Jordan kwa tauni ya ´Amwaas mwaka wa 18 baada ya kuhajiri akiwa na miaka 58.

[1] Abu Daawuud (4649) na (4650), at-Tirmidhiy (3748) na (3757), Ibn Maajah (134), Ahmad (1/187/189) na Ibn Abiy Aasim (1428), (1431) na (1436). al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni Swahiyh katika ”Swahiyh al-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (4010).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 145-146
  • Imechapishwa: 14/12/2022