Imamu haitikii ukumbusho wa maamuma wa kuswali Rak´ah tatu

Swali: Tuliswali nyuma ya imamu aliyeswali Dhuhr Rak´ah tatu ambapo tukamkumbusha lakini hakusimama. Kisha akasujudu sijda ya kusahau na baadhi ya wanaoswali wakasujudu pamoja naye na wengine hawakusujudu, bali waliinuka wakakamilisha Rak´ah ya nne na wakatoa salamu?

Jibu: Ni juu ya anayejua kuwa kuna upungufu alete Tasbiyh na amkumbushe. Akiinuka ni sawa. Vinginevyo wao wainuke na wakamilishe. Ama yeye afanyie kazi kwa ijtihadi yake; ikiwa anajua kuwa yuko sahihi, anakaa na kutoa salamu. Ama ikiwa hana uhakika, basi ni lazima awafuate wanaomkumbusha kwa Tasbiyh na kuzingatia onyo lao, asimame na alete Rak´ah ya nne. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokumbushwa katika moja ya swalah za ´Aswr kuwa alitoa salamu baada ya Rak´ah mbili, alisimama baada ya kuthibitisha kutoka kwao ambapo akakamilisha swalah. Vilevile katika Hadiyth ya pili, Hadiyth ya ´Imraan, alipokumbushwa kuwa ameswali Rak´ah tatu, alisimama na akaleta Rak´ah ya nne (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa hiyo ni wajibu juu ya imamu kufuata wanaomkumbusha kwa Tasbiyh na kufanyia kazi onyo lao. Ikiwa kuna upungufu, akamilishe, na ikiwa kuna ziada, arudi, isipokuwa ikiwa anajua kwa yakini kuwa yeye yuko sahihi na wao wamekosea. Katika hali hiyo afanyie kazi yakini yake.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3233/عدم-استجابة-الامام-لتسبيح-المامومين-حال-سهوه
  • Imechapishwa: 23/10/2026