Tumia muda wako katika vitabu vyenye faida na achana na vitabu visivyo na faida

Ni juu yako, ee ndugu yangu, kuielekea Qur-aan, kuisoma kwa wingi, kutafakari maana zake na kusimama katika Aayah zake na ujue makusudio ya Allaah ndani yake. Ikiwa jambo limekushinda, basi una vitabu vya tafsiri, rejea tafsiri za Qur-aan kama Ibn Jariyr, Ibn Kathiyr, al-Baghawiy, ash-Shawkaaniy, al-Qurtwubiy na wengineo. Miongoni mwa vilivyo na manufaa zaidi ni Ibn Jariyr, Ibn Kathiyr na al-Baghawiy.

Vilevile zirejee Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ufanikiwe nazo. Ikiwa wewe ni mwanafunzi ambaye uko na al-Bukhaariy, Muslim na vitabu vilivyofupishwa kama al-Muntaqaa´ cha Ibn Taymiyyah, ”Buluugh-ul-Maraam” cha Ibn Hajar, ”´Umdat-ul Ahkaam” cha ´Abd-ul-Ghaniy. Hivi vinakufaidisha, vitafakari, angalia mlango kuhusu swalah, zakaah, Tawhiyd na kadhalika, kisha waulize wanazuoni.

Ama vitabu visivyojulikana na usivyovijua hali yake, usipoteze muda wako ndani yako. Tumia muda wako katika vitabu vinavyojulikana kwa manufaa na kheri. Vilivyo bora zaidi ni Kitabu cha Allaah, kisha vitabu vya Sunnah kama vile al-Bukhaariy na Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah, ”al-Musnad” cha Ahmad.

Ikiwa wewe si mwanafunzi wa elimu, basi waulize wanazuoni na uzidishe kusoma Qur-aan na kuitafakari ili upate faida. Ama kutafuta vitabu vipya visivyojulikana hali yake na kupoteza muda humo, hapana. Ikiwa ni vitabu vizuri vilivyosifiwa na wanazuoni na ukaelekezwa navyo, basi hakuna ubaya kutumia muda wake, uchukue yaliyoafikiana na Qur-aan na Sunnah na uache yaliyo kinyume.

Watu wengine hupoteza muda wao katika majarida, magazeti, vitabu visivyo na thamani au vilivyojaa Bid´ah na upotofu au mambo yasiyo na faida. Sambamba na hilo wakiiacha Qur-aan yenye nuru na uongofu, Sunnah yenye nuru na uongofu na maneno ya wanazuoni wa haki. Hii ni njia ya upotofu:

فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ

“Hakika hayapofuki macho, bali zinazopofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.”[1]

[1] 22:46

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3239/لو-قرا-كتابا-ولم-يفهم-هل-تكون-عبادة-ام-ضياعا-للوقت
  • Imechapishwa: 12/10/2026