32. Wakati kifo kimeshahakikishwa

Inapohakikishwa kuwa mtu amekufa, macho yake hufumbwa na taya zake hufungwa. Isitoshe huwekwa juu ya tumbo lake kioo au kitu kingine kama chuma ili lisivimbe.

Anapoanza kumuosha, utupu wake hufunikwa. Kisha tumbo lake hubanwa kwa upole, kisha hujifunga kitambaa kwenye mkono wake na humuosha nacho sehemu zake za siri. Kisha humtawadhisha, kisha huosha kichwa na ndevu zake kwa maji na mkunazi, kisha upande wake wa kulia, kisha upande wake wa kushoto. Kisha humuosha hivyo hivyo mara ya pili na ya tatu. Kila mara hupitisha mkono wake juu ya tumbo lake. Ikiwa kitatoka kitu, hukiosha na kukiziba kwa pamba. Ikiwa hakishikamani, basi kwa udongo wa mfinyanzi safi. Kisha atamtawadhisha tena.

Ikiwa hatakuwa ametakasika kwa mara tatu, huongeza hadi mara tano au saba. Kisha humkausha kwa kitambaa na huweka manukato kwenye maficho yake na sehemu za kusujudia kwake. Ikiwa atampaka manukato mwili wake wote, hilo ni zuri. Sanda zake hufukizwa kwa udi. Ikiwa masharubu au kucha zake ni ndefu, basi hukatwa. Nywele zake hazichanwi.

Ama mwanamke, nywele zake husukwa mikia mitatu na hutupwa nyuma yake.

Kisha hufunikwa ndani ya nguo tatu nyeupe ambazo hazina kanzu wala kilemba na huviringishwa ndani yake. Hata hivyo hapana vibaya ikiwa atazikwa ndani ya kanzu, shuka ya chini na sanda.

Mwanamke huvikwa sanda ndani ya nguo tano: kanzu ya mwanamke, kitambaa cha kichwa, shuka ya chini na sanda mbili.

Watu walio na haki zaidi ya kumuosha maiti, kumswalia na kumzika ni wasii wake katika jambo hilo, kisha baba, kisha babu, kisha wa karibu zaidi na wa karibu zaidi miongoni mwa jamaa upande wa baba. Watu walio na haki zaidi ya kumuosha mwanamke ni mama yake, kisha bibi yake, kisha wa karibu zaidi na wa karibu zaidi miongoni jamaa zake wanawake zake. Isipokuwa kwamba mtawala hutangulizwa mbele katika kumswalia kuliko baba na wengineo.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 33
  • Imechapishwa: 18/10/2026