Ni faradhi kwa baadhi ya watu; ikiwa watu arobaini miongoni mwa wakazi wa mji wataitekeleza, basi huwa imeanguka kwa wengine wote.

Wakati wake ni kuanzia jua linapochomoza na kuinuka hadi wakati wa kupinduka. Sunnah ni kuiswali katika kiwanja. Swalah ya ´Iyd-ul-Adhwhaa´ inatakiwa kuharakishwa, na swalah ya ´Iyd-ul-Fitwr inatakiwa kucheleweshwa. Vilevile inatakiwa kula kabla ya swalah ya Fitwr.  Ni Sunnah kuoga, kujisafisha na kujipaka manukato.

Wakati swalah unapofika, basi imamu hutangulia mbele na kuwaswalisha Rak´ah mbili bila adhaana wala iqaamah. Katika Rak´ah ya kwanza ataleta Takbiyr saba pamoja na ile Takbiyr ya kufungulia swalah. Katika Rak´ah ya pili ataleta Takbiyr tano, bila kuhesabu ile Takbiyr kwa ajili ya kusimama katika Rak´ah ya pili.

Hunyanyua mikono yake pamoja na kila Takbiyr. Humhimidi Allaah na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baina ya kila Takbiyr mbili. Kisha husoma al-Faatihah na Suurah nyingine. Husoma kwa sauti ya juu katika zote mbili.

Wakati imamu anapotoa salamu, huwakhutubia kwa Khutbah mbili. Ikiwa ni ´Iyd-ul-Fitwr, basi huwahimiza kutoa swadaqah na kuwaelezea hukumu zake. Ikiwa ni ´Iyd-ul-Adhwhaa´, basi huwaelezea hukumu zinazohusiana na Udhhiyah. Takbiyr za ziada na Khutbah mbili ni mambo yanayopendeza.

Hakuswaliwi swalah ya kujitolea kabla ya swalah ya ´Iyd wala baada yake katika mahali pake. Mwenye kumuwahi imamu kabla hajatoa salamu, basi ataikamilisha kwa namna yake. Ambaye hakumuwahi, halazimiki kuilipa. Lakini akipenda, anaweza kuiswali kama swalah ya kujitolea; akitaka Rak´ah mbili, akitaka nne na akitaka ataiswali kwa namna yake.

Inapendeza kuleta Takbiyr katika zile nyusiku mbili za kuamkia siku mbili za ´Iyd. Katika yale masiku ya ´Iyd-ul-Adhwhaa ataleta Takbiyr baada ya swalah za faradhi za mkusanyiko kuanzia swalah ya Fajr ya siku ya ´Arafah hadi ´Aswr ya siku ya mwisho ya Tashriyq. Isipokuwa aliye ndani ya Ihraam, yeye huleta Takbiyr kuanzia swalah ya Dhuhr ya siku ya kuchinja hadi ´Aswr ya siku ya mwisho ya Tashriyq. Namna ya Takbiyr ni kama ifuatavyo:

الله أكبر الله أكبر، لا اله إلا الله، و الله أكبر الله أكبر، و لله الحمد

“Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaa. Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa. Himdi zote njema ni za Allaah.”

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 32
  • Imechapishwa: 18/10/2026