Kila mwenye kulazimika kuswali swalah ya faradhi, anawajibikiwa na swalah ya ijumaa ikiwa ni mkazi wa kudumu katika majengo na kati yake na msikiti wa ijumaa kuna umbali usiyopungua Farsakh moja[1]. Isipokuwa mwanamke, mtumwa, msafiri na mwenye udhuru kwa ugonjwa, mvua au khofu. Ikiwa watahudhuria ijumaa, basi swalah yao inasihi. Lakini ijumaa haisimami kwa uwepo wao, isipokuwa mwenye udhuru akihudhuria, basi hapo ijumaa inakuwa ni wajibu kwake na inasimama kwa uwepo wake.

Miongoni mwa masharti ya kusihi kwake ni kuswaliwa katika wakati wake katika kijiji, kuhudhuriwa na watu arobaini miongoni mwa wakazi wake ambao wanawajibikiwa na ijumaa na kutanguliwa na Khutbah mbili. Katika kila Khutbah kuwe na kumhimidi Allaah (Ta´ala), kumswalia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kusoma Aayah za Qur-aan na kutoa mawaidha.

Inapendekezwa imamu akhutubie juu ya mimbari. Anapopanda, basi huwaelekea watu na kuwapa salamu, kisha hukaa mpaka adhaana imalizike. Kisha imamu husimama na kuwakhutubia, kisha hukaa, halafu hutoa Khutbah ya pili. Kisha swalah husimamishwa, naye hushuka na kuwaswalisha Rak´ah mbili, akisoma ndani yake kwa sauti ya juu.

Mwenye kuwahi Rak´ah moja pamoja naye, basi anaikamilisha hali ya kuwa ijumaa. Asipowahi, basi anaikamilisha hali ya kuwa Dhuhr. Vivyo hivyo ikiwa idadi ya watu itapungua au wakati ukatoka baada ya wao kuswali Rak´ah moja, basi wanaikamilisha hali ya kuwa ijumaa. Ikiwa hawajawahi Rak´ah moja, wanaikamilisha hali ya kuwa Dhuhr.

Haijuzu kuswaliwa swalah ya ijumaa zaidi ya moja katika mji mmoja, isipokuwa ikiwa kuna haja inayohitaji kufanya zaidi ya moja.

Inapendekezwa kwa mwenye kwenda kuswali swalah ya ijumaa kuoga, kuvaa nguo mbili safi, kujipaka manukato na kwenda mapema. Akija huku imamu akikhutubu, basi asikae mpaka aswali Rak´ah mbili ambazo azifupishe.

Haijuzu kuzungumza wakati imamu akikhutubu, isipokuwa imamu mwenyewe au mtu ambaye imamu amemzungumzisha.

[1] Takriban mita 5544.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 18/10/2026