Mgonjwa ikiwa kusimama kunamzidishia ugonjwa wake, basi ataswali akiwa amekaa. Ikiwa hawezi, ataswali akiwa amelala kwa ubavu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh):

“Swali ukiwa umesimama. Ikiwa huwezi, basi ukiwa umekaa. Ikiwa huwezi, basi ukiwa kwa ubavu wako.”[1]

Ikiwa kufanya hivyo kutamletea uzito, basi ataswali akiwa amelala chali. Ikiwa hawezi kurukuu na kusujudu, basi ataashiria kwa ishara.

Anawajibika kulipa swalah alizozikosa alipokuwa amezimia.

Ikiwa ni uzito kwake kuswali kila swalah katika wakati wake, basi anaruhusiwa kukusanya Dhuhr na ´Aswr, na kadhalika Maghrib na ´Ishaa katika wakati wa mojawapo ya hizo. Akikusanya katika wakati wa swalah ya kwanza, basi ni lazima awe na nia ya kujumuisha wakati wa kuanza kuiswali. Udhuru huo uendelee mpaka aanze swalah ya pili kati ya hizo mbili. Wala asitenganishe kati ya swalah hizo mbili isipokuwa kwa muda wa kutawadha. Ikiwa atachelewesha kukusanya katika ile swalah ya pili, basi ni sharti udhuru huo uendelee mpaka uingie wakati wa swalah ya pili, na pia anuie kukusanya katika wakati wa swalah ya kwanza kabla ya wakati wake kuwa mfinyu kiasi cha kutotosha kuiswali.

Inajuzu pia kukusanya kwa msafiri ambaye anaruhusiwa kufupisha swalah, na vilevile inajuzu kukusanya Maghrib na ´Ishaa kwa sababu ya mvua.

[1] al-Bukhaariy (1117).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 18/10/2026