Abu Mas´uud al-Badriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Awaongoze watu katika swalah yule anayesoma vizuri zaidi Kitabu cha Allaah. Ikiwa wako sawa katika usomaji, basi yule mjuzi zaidi katika wao juu ya Sunnah. Ikiwa wako sawa katika Sunnah, basi aliyetangulia zaidi katika Hijrah. Ikiwa wako sawa katika Hijrah, basi awaongoze mkubwa wao kwa umri. Mtu asimuongoze mtu mwingine katika nyumba yake wala katika mamlaka yake, wala asikae katika sehemu yake ya heshima isipokuwa kwa idhini yake.”[1]

Alimwambia Maalik bin al-Huwayrith na mwenzake:

“Swalah inapowadia, basi mmoja wenu atoe adhaana na mkubwa wenu awaongoze.”[2]

Usomaji wao ulikuwa unakaribiana.

Swalah haisihi nyuma ya mtu ambaye swalah yake ni yenye kuharibika, isipokuwa yule ambaye hajui kwamba ametokwa na hadathi, na maamuma pia hakujua hilo mpaka imamu akatoa salamu. Katika hali hiyo maamuma ataswali tena peke yake.

Haisihi kuswali nyuma ya mtu anayeacha nguzo, isipokuwa imamu wa kudumu wa msikiti anaposwali akiwa amekaa kwa sababu ya ugonjwa unaotarajiwa kupona. Katika hali hiyo wao huswali nyuma yake wakiwa wamekaa. Isipokuwa ikiwa alianza swalah akiwa amesimama, kisha akapatwa na ugonjwa akakaa. Katika hali hiyo wao humfuata wakiwa wamesimama.

Haisihi mwanamke kuwaswalisha wanaume. Wala haisihi kwa yule mwenye maradhi ya kutokwa hovyo na mkojo na mtu asiyeweza kusoma vizuri al-Faatihah au anayeharibu herufi yoyote ndani yake. Hawawezi kuwa imamu isipokuwa kwa watu walio katika hali kama yao.

Inajuzu mwenye kutawadha kuswalishwa na mtu aliyefanya Tayammum. Inajuzu pia mwenye kuswali faradhi kuswalishwa na mwenye kuswali swalah ya kujitolea.

Ikiwa yule anayeswalishwa ni mmoja, atasimama upande wa kuliani mwa imamu. Akiwa amesimama upande wake wa kushoto, mbele yake au sambamba naye, basi swalah haisihi. Isipokuwa ikiwa yule anayeswalishwa ni mwanamke ambaye atasimama peke yake nyuma yake.

Ikiwa wale wanaoswalishwa ni kundi la watu, watasimama nyuma yake. Wakisimama upande wake wa kulia au pande zake mbili, swalah inasihi. Wakisimama mbele yake au upande wake wa kushoto, swalah haisihi.

Ikiwa mwanamke atawaongoza wanawake wenzake, atasimama pamoja nao katikati ya safu. Vivyo hivyo imamu wa wanaume walio uchi atasimama katikati yao.

Ikiwa wamekusanyika wanaume, watoto, wenye jinsia mbili na wanawake, basi watatangulizwa mbele wanaume, kisha watoto, kisha wenye jinsia mbili, kisha wanawake.

Yule mwenye kuleta Takbiyr kabla ya imamu kutoa salamu, basi amewahi swalah ya mkusanyiko. Yule mwenye kuwahi Rukuu´, amewahi Rak´ah. Vinginevyo, hajapata.

[1] Muslim (673).

[2] al-Bukhaariy (628) na Muslim (674).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 12/10/2026