Aina zake ni tano:

1 – Sunnah zinazopendeza zinazoswaliwa katika mnasaba wa swalah za faradhi. Hizi ndizo alizozisema Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Rak´ah kumi nilizozihifadhi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): Rak´ah mbili kabla ya Dhuhr, Rak´ah mbili baada yake, Rak´ah mbili baada ya Maghrib nyumbani kwake, Rak´ah mbili baada ya ´Ishaa nyumbani kwake na Rak´ah mbili kabla ya Fajr.”[1]

Amesema tena:

“Hafswah alinisimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipopambazuka Fajr na muadhini akatoa adhaana, aliswali Rak´ah mbili.”[2]

Hizi ndizo zilizosisitizwa zaidi. Inapendekezwa kuzifanya kwa ufupi. Isitoshe kuziswali nyumbani ndio bora. Vivyo hivyo Rak´ah mbili za Maghrib.

2 – Witr. Wakati wake ni kati ya swalah ya ´Ishaa na Fajr. Rak´ah zake chache ni moja, na wingi wake ni kumi na moja. Kiwango cha chini cha ukamilifu ni Rak´ah tatu kwa Tasliym mbili. Qunuut inasomwa katika Rak´ah ya tatu baada ya Rukuu´.

3 – Swalah ya kujitolea isiyofungamanishwa. Swalah ya usiku ndio bora kuliko ya mchana. Nusu ya mwisho ya usiku ndio bora kuliko nusu ya kwanza. Swalah ya usiku huswaliwa Rak´ah mbilimbili. Swalah ya mwenye kukaa malipo yake ni nusu ya swalah ya mwenye kusimama.

4 – Swalah ambazo inapendekezwa kuswaliwa kwa mkusanyiko. Nazo ni aina tatu:

1 – Taraawiyh, nazo ni Rak´ah ishirini baada ya ´Ishaa katika Ramadhaan.

2 – Swalah ya kupatwa kwa jua. Jua au mwezi unapopatwa, watu hukimbilia swalah. Wakipenda huswali kwa mkusayiko, watafanya hivo, na wakipenda huswali mmojammoja, watafanya hivo. Huleta Takbiyr na kusoma al-Faatihah pamoja na Suurah ndefu, kisha hurukuu Rukuu´ ndefu. Kisha huinuka na kusoma al-Faatihah pamoja na Suurah ndefu ambayo ni fupi kuliko ile ya kwanza. Kisha hurukuu na kurefusha Rukuu´ hiyo, lakini iwe fupi kuliko Rukuu´ iliyotangulia. Kisha huinuka, halafu husujudu sijda mbili ndefu. Kisha husimama na kufanya kama alivyofanya hapo awali. Hivyo huwa ni Rak´ah nne na sijda nne.

3 – Swalah ya kuomba mvua. Ardhi inapokumbwa na ukame na mvua ikazuilika, basi watu hutoka pamoja na imamu wakiwa wanyenyekevu, wamevaa mavazi ya kawaida, wanyenyekevu na wenye kumuomba Allaah kwa unyenyekevu. Huwaswalisha Rak´ah mbili kama swalah ya ´Iyd, kisha huwakhutubia Khutbah moja. Huomba msamaha kwa wingi na kusoma Aayah ambazo ndani yake kuna amri ya kuomba msamaha. Watu hugeuza nje-ndani mavazi yao ya juu. Ikiwa Wale walipa kodi ya ulinzi watatoka pamoja nao, hawazuiwi. Hata hivyo wanaamrishwa kujitenga na waislamu.

5 – Sijda ya kisomo. Ni sijda kumi na nne, zikiwemo mbili katika Suurah al-Hajj. Inapendekezwa msomaji na anayesikiliza kwa makusudi kusujudu. Hata hivyo si lazima kwa anayesikia bila kukusudia. Huleta Takbiyr anaposujudu na anapoinua kichwa chake, kisha hutoa Tasliym.

[1] al-Bukhaariy (1180) na Muslim (729).

[2] al-Bukhaariy (1181) na Muslim (723).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 12/10/2026