Swali: Je, ni haramu kuswali ndani ya msikiti wenye kaburi kama vile msikiti wa al-Husayn na bibi Zaynab? Ukifika wakati wa swalah na hakuna msikiti mwingine karibu inafaa kuswali ndani yake?

Jibu: Haifai kuswali ndani ya misikiti yenye makaburi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani watu wa misikiti yenye makaburi:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia. Zindukeni! Msiyafanye makaburi kuwa ni mahali pa kuswalia, hakika ,imi nakukatazeni hilo.”[1]

Ikiwa umepata msikiti wenye kaburi peke yake swali nyumbani kwako. Tafuta msikiti usiokuwa na kaburi. Ikiwa misikiti yote iko na makaburi swali nyumbani kwako pamoja na ndugu zako wazuri mpaka pale mtapopata msikiti wa Ahl-us-Sunnah uliosalimika. Kuhusu msikiti wenye makaburi hakuswaliwi ndani yake. Ni mamoja Misri au mahali kwengine kokote.

Swali: Wako wanaosema kuwa aswali ndani yake na afikishe ujumbe?

Jibu: Hapana, asiswali ndani yake. Awafikishie ujumbe pasi na kuswali nao. Asiswali nao. Awaendee baada ya swalah. Vinginevyo awasubiri watajapomaliza kuswali awafunze ya kwamba haifai kuswali katika msikiti huo na kwamba ni maovu. Anatakiwa kuwafunza. Kusema kwamba awafuate katika batili asifanye hivo.

Swali: Kukisemwamba kwamba usulubu huu unawakimbiza watu?

Jibu: Hapana. Yale yaliyofanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayakimbizi watu mbali. Kinachokimbiza watu ni kwenda kinyume na Sunnah. Lakini kwenda sambamba na Sunnah hakukimbizi watu.

[1] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/23126/هل-الصلاة-في-مسجد-به-قبر-حرام
  • Imechapishwa: 19/11/2023