Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho basi azungumze kheri au anyamaze.”[1]

Je, makusudio ni kwamba kwa mfano akiwa katika kikao ambacho kuna usengenyi awanyamazie au ashirikiane nao?

Jibu: Maneno yake (´alayhis-Salaam):

“… azungumze kheri.”

akemee. Akiwasikia awakemee na kuwakumbusha wamche Allaah na kwamba waache kusengenya. Vivyo hivyo akiwa katika kikao ambacho kuna umbea. Ikiwa kuna pombe awakataze. Ikiwa ndani yake kuna uzinzi awakataze. Namna hii akiona maovu ayakemee. Vinginevyo atengane nao na kujiweka mbali. Asiketi nao juu ya maovu.

Swali: Au abadilishe mada?

Jibu: Hapana. Ni lazima akemee maovu pamoja na kubadilisha mada. Jambo la kukemea maovu ni la lazima:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu.”[2]

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu – mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.”[3]

Ametanguliza kuamrisha na kukemea kabla ya kumwamini Allaah ili kuonyesha ukubwa wa jambo hilo.

Swali: Ni jambo gumu anapokuwa katika kikao cha watu wakubwa kuwaambia…

Jibu: Haki ni kubwa zaidi kuliko wao. Haki ni kubwa zaidi. Kwa ajili hiyo wakati ´Abdullaah bin ´Umar alipoona aibu kuzungumza kuhusu mti wa mtende, baba yake ´Umar akamwambia:

“Ungelikuwa umesema kungelipendeza zaidi kwangu kuliko kadhaa na kadhaa.”

Mtu asiidharau nafsi yake kutokana na kheri. Akemee maovu hata kama ndiye mdogo kabisa wa watu.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

[2] 09:71

[3] 03:110

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/23153/معنى-فليقل-خيرا-او-ليصمت-في-الحديث
  • Imechapishwa: 19/11/2023