Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  amesema:

“Miongoni mwa sifa nzuri za muislamu ni kuachana na yale yasiyomuhusu.”

Hadiyth ni nzuri. Ameipokea at-Tirmidhiy na wengine.

Usiingilie mambo ya watu ikiwa hayakuhusu. Hili ni kinyume na yale yanayofanywa na baadhi ya watu leo. Utaona baadhi kuna watu wenye kupupia kutaka kuvunja heshima na hali za watu. Anajaribu kuwajongelea watu wawili anaowaona wanazungumza ili aweze kusikia wanayosema.Wakati anamuona mtu anatoka upande fulani, utaona anapeleleza [kutaka kujua alipotoka]. Huenda akamwendea kwa haraka huyo mtu mwenyewe na kumuuliza alipotoka, fulani amemwambia nini, ulimwambia nini na mfano wa hayo. Anamuuliza mambo yasiyomuhusu. Achana na mambo yasiyokuhusu. Hakika kufanya hivo ni moja miongoni mwa sifa nzuri za Uislamu wako. Isitoshe kufanya hivo kuna kumpumzisha mwanadamu. Kule mtu kutojishughulisha na ya wengine isipokuwa yanayomuhusu tu, huku ndio kupumzika. Ama kuhusu yule mtu mwenye kupeleleza hali za watu na anataka kujua kila kilichopitika na kusemwa, mtu huyu hutaabika sana na hupitwa na mambo ya kheri mengi. Pamoja na yote haya hafaidi lolote.

Tazama yanayokuhusu na kukunufaisha nafsi yako. Kile kinachokupa manufaa, kifanye. Kile kisichokupa manufaa, achana nacho. Hii sio miongoni mwa sifa nzuri za Uislamu wako kupekua yasiyokuhusu.

Lau tungelitendea kazi haya na ikawa mtu haangalii isipokuwa mambo yake tu, basi kungelipatikana kheri nyingi.

Ama baadhi ya watu utawaona wameshughulishwa tu na mambo ya wengine katika mambo ambayo hayana faida yoyote na yeye. Hili linapelekea kupoteza wakati wake, kuushughulisha moyo wake, kuzichosha fikira zake na kupitwa na mambo mengi yenye faida.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/510-511)
  • Imechapishwa: 25/06/2023