01. Watu wote wanalingana, watu wote wanatofautiana

Kundi hili linasema ambaye anayatambua yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah na akatamka shahaadah ya kweli kwa ulimi wake, basi hiyo ndio imani yote, kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amewaita waumini.

Kutokana na vile tunavyoona ´Aqiydah yao si chochote na hilo ni kwa sababu ya mambo mawili:

1 – Umekwishajua tangu hapo mwanzo kwamba imani ya faradhi mwanzoni mwa Uislamu ilikuwa inahusiana na kutambua peke yake.

2 – Watu hupata majina kutokana na ule mwanzo na kuingia kwao. Baada ya hapo ndio wakashindana na kutofautiana. Wote wamekusanywa na jina moja. Utaona kundi la watu wamesimama katika safu kuswali; wanafunga swalah, wanarukuu na wanasujudu, wanasimama na kuketi chini. Wote wanaitwa waswaliji. Pamoja na hivo ni wenye kutofautiana katika swalah zao.

Mfano mwingine ni kundi la wajenzi wanaojenga ukuta; baadhi yao wanaanza na msingi wake, wengine wakachukua ile sehemu yake ya katikati na wengine wakachukua ile sehemu yake ya juu ya kumalizia. Wote wanaitwa kuwa ni wajenzi, lakini kazi zao zinatofautiana.

Mfano mwingine ni kama kundi la watu wataamrishwa kuingia nyumba fulani; mmoja wao akaingia na kusimama ndani ya kizingiti, wa pili akazidi kwa hatua chache, na wa tatu akatembea mpaka katikati ya nyumba. Kutasemwa kuwa wote wameingia ndani, lakini baadhi yao wameingia zaidi kuliko wengine.

Mifano hii ni yenye kutambulika kwa waarabu.

Vivyo hivyo kuhusu imani; inahusiana na kuingia ndani ya dini. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّـهِ وَالْفَتْحُ وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّـهِ أَفْوَاجًا فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا

”Itakapokuja nusura ya Allaah na ushindi na ukawaona watu wanaingia katika dini ya Allaah makundi kwa makundi. Basi hapo tukuza na muhimidi Mola wako na muombe msamaha. Hakika Yeye daima ni Mwingi mno wa kupokea tawbah.”[1]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ

“Enyi mlioamini! Jisalimisheni kikamilifu na wala msifuate hatua za shaytwaan – hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.”[2]

Kwa mujibu wa waarabu maana yake ni mtu kuingia ndani ya Uislamu kikamilifu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengeka juu ya mambo matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba.”[3]

Nguzo zote hizi tano zikawa ni Uislamu ambayo Allaah ameita kuwa ni Uislamu uliofaradhishwa.

Kwa maana nyingine tunaona matendo mema, ufundi na kuingia majengo vyote vinaingia katika jina moja, lakini ngazi zao zinatofautiana. Huku ni katika kufananisha peke yake; vinginevyo tumekwishajengea hoja ya Qur-aan na Sunnah. Vivyo hivyo kuhusu imani. Ina daraja na ngazi mbalimbali ijapo wenye nayo wanaitwa jina moja. Imani ni kitendo ambacho Allaah amewafaradhishia waja Wake kumwabudu. Ameifaradhisha imani kwa viungo vyao vya mwili, akafanya msingi wake katika utambuzi wa moyo kisha akafanya kule kutamka kukashuhudia jambo hilo na matendo kuisadikisha. Allaah amekipa kila kiungo cha mwili kitendo maalum kinachoendana. Matendo ya moyoni ni kule kuitakadi. Matendo ya ulimi ni kauli. Matendo ya mkono ni kule kupokea. Matendo ya mguu ni kule kutembea. Yote haya yanakusanywa na jina matendo. Kutokana na haya imani yote imejengeka juu ya matendo, kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake. Hata hivyo inatofautiana kama tulivyosema.

[1] 110:1-3

[2] 2:208

[3] al-Bukhaariy (08) na tamko ni lake, na Muslim (16).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 49-53
  • Imechapishwa: 26/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy