Swali: Kipindi cha mwisho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanyiwa utovu wa adabu kwa mara zenye kukariri kupitia filamu, magazeti na njia nyenginezo. Ni upi msimamo wa Kishari´ah juu ya utovu wa adabu huu? Ni ipi hukumu mtu akaonesha hasira zake dhidi ya utovu wa adabu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kufanya maandamano?

Jibu: Ndugu! Haya si mapya. Yalikuweko wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walisema kuwa ni mchawi, mwongo, kuhani, mshairi na mengineyo. Licha ya hivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasubiri. Alikuwa akivuta subira na wala hafanyi haraka. Allaah alikuwa akimwamrisha kufanya subira:

وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا

“Subiri juu ya yale wayasemayo na wahame muhamo mzuri.”[1]

Anasikia, lakini hata hivyo anafanya subira kutokana na amri ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

“Kwa hakika Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kutokana na yale wanayoyasema. Basi tukuza kwa himdi za Mola wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu na mwabudu Mola wako mpaka kikufikia kifo.”[2]

Alikuwa anasubiri na anawakataza Maswahabah zake asiweko yeyote ambaye atalipiza kisasi pindi walikuweko Makkah. Lau wangelipiza kisasi juu ya washirikina basi Uislamu na Da´wah ambayo ilikuwa bado changa vingelitokomea. Mpaka pale alipohama na akapata msaada wa wanusuraji ndipo Allaah alimwamrisha kuwapiga vita washirikina. Ilikuwa Jihaad ya Kishari´ah.

Kuhusu maandamano, maharibifu na kuwaua watu wasiokuwa na hatia na watu ambao wanaishi chini ya usalama na ulinzi wa waislamu, ni usaliti usiofaa. Haijuzu kuwaua watu wasiokuwa na hatia ijapokuwa ni makafiri. Haijuzu:

وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ أَن صَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ أَن تَعْتَدُوا

“Wala isikupelekeeni chuki juu ya watu kwa vile walikuzuieni kutokamana na al-Masjid al-Haraam mkachupa mpaka.”[3]

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ

“Wala habebi mbebaji mzigo [wa dhambi] wa mtu mwengine.”[4]

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ

“Ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka ayasikie maneno ya Allaah kisha mfikishe mahali pake pa amani.”[5]

Wajumbe wa washirikina walikuwa wakimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikuwa wanaingia mpaka ndani msikitini mwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alipatana nao ingawa ni washirikina na makafiri. Lakini inapaswa itambulike kuwa Uislamu sio dini ya hasira na dini ya kulipiza kisasi. Uislamu ni dini ya uongofu, huruma na upole, kama alivokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Natija ilikuwa ipi? Hatimaye Allaah alimnusuru Mtume Wake na akaitukuza dini Yake na wale ambao walikuwa wakimchezea shere Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baadhi yao wakawa ndio viongozi wa Uislamu na wapambanaji katika njia ya Allaah. Wakaingia ndani ya Uislamu na wakaufanya vizuri Uislamu wao kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwavumilia na akawafanyia upole na urafiki. Yakapelekea mpaka wakaanza kumpenda. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ

”Hakika wewe bila shaka una tabia nzuri mno.”[6]

Hii ndio ilikuwa tabia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Pindi makafiri wanapofanya matendo haya makusudio yao ni kuchokoza. Wanasema:

“Tazama wanayofanya waislamu! Wanaua mabalozi! Wanaharibu na kubomoa majengo! Je, haya ndio Uislamu?”

Hii ndio ajenga ya makafiri. Wanataka iwe matokeo mabaya kwa waislamu kutokanaa na matendo mabaya ya waislamu wajinga au pengine wale waliopandikizwa na wao. Haifai kufanya papara katika mambo haya:

وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا وَأُوذُوا حَتَّىٰ أَتَاهُمْ نَصْرُنَا ۚ وَلَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِ اللَّـهِ ۚ وَلَقَدْ جَاءَكَ مِن نَّبَإِ الْمُرْسَلِينَ

“Kwa hakika walikadhibishwa Mitume kabla yako wakasubiri juu ya yale waliyokadhibishwa na wakaudhiwa mpaka ilipowafikia nusura Yetu; na hakuna abadilishaye maneno ya Allaah. Tayari zimekwishakujia khabari za Mitume.”[7]

Namna hii ndivo unahimiza Uislamu namna ya kutaamiliana na mambo haya. Upole, kuyapima mambo na subira na kutokuwa na papara.

Washirikina wanatakiwa kutumia fursa kwa mambo haya kutokana na yatayotokea kutoka kwa baadhi ya waislamu kama vile majivuno, maharibifu na mauaji. Mwishowe waislamu wao kwa wao waanze kupigana vita. Wafanya maandamano wataanza kupigana vita na walinzi wa amani. Hii ndio ajenga ya makafiri.

[1] 73:10

[2] 15:97-99

[3] 05:02

[4] 06:164

[5] 09:06

[6] 68:04

[7] 06:34

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alfawzan.af.org.sa/node/14100 Tarehe: 1433-11-07/2012-09-23
  • Imechapishwa: 28/08/2020