Ni haramu au imechukizwa kutembea na viatu makaburini?

Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee uliye na viatu vya ngoz! Vua viatu vyako. Kwani hakika umeudhi.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza vilevile mwanaume kuchana nywele kila siku. Udhahiri wa Hadiyth ya kwanza ni uwajibu na ya pili ni uharamu. Lakini kuna wanachuoni wenye kusema Hadiyth ya kwanza ni jambo limependekezwa na ya pili ni jambo limechukizwa bila ya kutaja dalili ya hukumu hizo mbili. Ni maoni yepi unayoonelea ndio yenye nguvu?

Jibu: Hiyo sehemu ya mwisho katika Hadiyth siijui:

“Ee uliye na viatu vya ngoz! Vua viatu vyako. Kwani hakika umeudhi.”

Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa imechukizwa kutembea na viatu makaburini. Nami naonelea kuwa maoni haya ndio yenye nguvu kuliko yale maoni yanayoharamisha, kwa kuwa makatazo yanahusiana na kuyatukuza na kuyaheshimisha makaburi ya waislamu. Naonelea kuwa maoni yanayosema kuwa imeharamishwa kwa kuwa ni kuyatweza makaburi ya waislamu hayako wazi. Haya ndio yaliyofanya kitendo hicho kiwe ni chenye kuchukiza.

Kuhusu makatazo ya [mwanaume] kuchana kila siku, ni maelekezo ya kujiepusha na anasa na kupoteza muda.

 Wanachuoni wa misingi wametofautiana kama amri ina uwajibu na katazo lina uharamu. Kuna maoni matatu juu ya suala hili:

1 – Amri ina uwajibu. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Watahadhari wale wanaokwenda kinyume na amri yake isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[1]

Amri inapelekea katika uharamu. Allaah (Ta´ala):

وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا

“Anayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika amepotoka upotofu wa wazi.”[2]

2 – Amri ina mapendekezo kwa kuwa uamrishaji unategemea kitendo chenyewe. Asli ni kutakasika dhimma na hakuna dhambi kwa kuacha kitendo. Matishio katika Aayah yanahusu yale maamrisho ambayo uwajibu wake umethibiti na sio maamrisho yote.

Makatazo yana machukizo kwa kuwa makatazo yanategemea kule kuacha. Asli ni kuwa kutokupata dhambi kwa kutenda. Hii ndio maana hakika ya machukizo. Kusema kwamba mtenda maasi katika Aayah amepotea upotevu wa wazi kunamaanishwa yule anayetenda maasi. Inaweza pia kusemwa, ijapokuwa tafsiri iko mbali, ya kwamba upotevu ni kukhalifu uongofu; inaweza kuwa maasi na inaweza pia kuwa chini ya hapo. Jibu hili ni dhaifu.

3 – Ikiwa amri inahusiana na adabu basi ni ya mapendekezo. Ikiwa amri inahusiana na adabu basi ni ya machukizo. Ikiwa amri inahusiana na ´ibaadah basi ni ya uwajibu na ya uharamu. Katika hali ya kwanza inahusiana na muruwa, katika hali ya pili inahusiana na Shari´ah.

Tofauti hii inafanya kazi midhali hakuna dalili yoyote inayoashiria uwajibu, mapendekezo, machukizo au uharamu. Ikiwa kuna dalili ya uwajibu, mapendekezo, machukizo au uharamu inatendewa kazi.

[1] 24:63

[2] 33:36

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/200-202)
  • Imechapishwa: 23/08/2021