´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 11: Shirki ni nini na imegawanyika aina ngapi?

Jibu: Kuna sampuli mbili za shirki:

1 – Shirki katika uola. Ina maana ya mtu kuamini kuwa Allaah yuko na mshirika katika kuumba au kuendesha baadhi ya viumbe.

2 – Shirki katika ´ibaadah. Shirki hii imegawanyika katika shirki kubwa na shirki ndogo.

Shirki kubwa maana yake ni mtu kumtekelezea aina moja miongoni kwa aina za ´ibaadah akamtekelezea asiyekuwa Allaah. Kwa mfano mtu akamuomba mwengine asiyekuwa Allaah, akamtarajia au akamuogopa. Hili linamtoa mtu katika dini na linamfanya mwenye nayo kudumishwa Motoni milele.

Kuhusiana na shirki ndogo, ni sababu na njia inayopelekea katika shirki ambayo sio ´ibaadah. Mfano wa hilo ni kama kuapa kwa asiyekuwa Allaah, kujionyesha na mfano wa hayo.

MAELEZO

1 – Shirki katika utendakazi wa Allaah ni ndogo ukilinganisha na shirki katika ´ibaadah. Wale wanaomkanusha Allaah na wakadai kwamba wameumbwa na maumbile wanaitwa “wanakamungu”. ´Aqiydah hii walikuwa nayo umoja wa Kisovyeti na nchi nyenginezo zilizowafuata katika ´Aqiydah hii.

Vivyo hivyo baadhi ya Suufiyyah wamewafuata katika shirki hiyo. Wanaamini kuwa wapo baadhi ya mawalii wanaoendesha ulimwengu. Ametakasika Allaah, Aliye mtukufu, kutokamana na mapungufu! Watu hawa ndio wenye kushirikisha katika uola. Pamoja na kwamba shirki katika uola haikuwepo katika zama za kale isipokuwa kwa watu wachache mno. Wengi ambao wanakanusha uwepo wa Allaah ndio ambao wanaamini uwepo Wake ndani ya nafsi zao. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Fir´awn na watu wake:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا ۚ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ

“Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha kwa dhulma na majivuno; basi tazama vipi ilikuwa hatima ya mafisadi.”[1]

Kushirikisha katika uola kunaingia vilevile kushirikisha katika majina na sifa. Wale wanaokanusha majina na sifa za Allaah zinazothibitisha ukamilifu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa njia inayolingana na utukufu Wake kama mfano wa Jahmiyyah, Mu´tazilah na vifaranga vyao. Wanaingia vilevile  wale wanaozipindisha sifa za Allaah (´Azza wa Jall) japo madhara yao ni madogo kuliko hao wa mwanzo. Ashaa´irah hawathibitishi isipokuwa tu sifa saba. Sifa zengine zote wanazipindisha. Kwa njia hiyo wao ni Jahmiyyah kwa sababu wanapinga maana ya sifa zengine zote.

2 – Kushirikisha katika ´ibaadah. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu.”[2]

Shirki kubwa ni mja kufanya aina moja wapo ya ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah. Kama mfano wa kumwomba mwengine asiyekuwa Allaah, kumtarajia mwengine asiyekuwa Allaah au kumwogopa mwengine khofu ya aina ya ´ibaadah kwa asiyekuwa Allaah.

Kadhalika yule mwenye kujikurubisha kwa kiumbe kwa madai kwamba ni walii na akaamini kuwa ana uwezo wa kunufaisha na kuzuia madhara kutoka kwa waja. Matokeo yake akajikurubisha kwao kwa kumwaga damu, akawachinjia, akayazunguka makaburi yao na akawaomba yale asiyoombwa mwengine isipokuwa Allaah pekee.

Kwa kifupi ni kwamba yule mwenye kufanya kitu katika aina za ´ibaadah akamfanyia mwengine asiyekuwa Allaah amemshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na amempa kitu asichostahiki. Kwa ajili hiyo anastahiki kutoka nje ya Uislamu na kuhukumiwa kwamba akifa katika hali hiyo basi atadumishwa Motoni milele.

Khofu imegawanyika aina mbili:

1 – Khofu ya kimaumbile.

2 – Khofu ya ki-´Ibaadah.

Yule mwenye kudai kwamba walii fulani anamjua yule anayemzungumza na humpatiliza ambapo akamwogopa, katika hali kama hii anazingatiwa kuwa ni mshirikina amefanya shirki kubwa yenye kumtoa nje ya Uislamu.

Kuhusu shirki ya kimaumbile ambapo mtu akamwogopa adui yake asije kumdhuru au asimuue au akaogopa simba, mbwamwitu au nyoka. Woga kama huu wote ni wa kimaumbile. Ni woga unaofaa. Hata hivyo haitakikani kwa mtu akachupa mpaka. Muislamu anatakiwa kumwomba Allaah amlinde kutokamana na woga na yale yote yanayohusiana nao.

Kuhusu shirki ndogo mtunzi wa kitabu amesema:

“Kuhusiana na shirki ndogo, ni sababu na njia inayopelekea katika shirki ambayo sio ´ibaadah. Mfano wa hilo ni kama kuapa kwa asiyekuwa Allaah, kujionyesha na mfano wa hayo.”

Miongoni mwa shirki ndogo kunaingia pia kujionyesha ambapo kunayapata matendo. Vilevile kuna kujionyesha kuliko nyuma ya matendo. Kujionyesha sampuli hii ndivo wafanyavo wanafiki na ni shirki kubwa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu.”

Ambaye hasimami kwa ajili ya swalah isipokuwa kwa kuwaogopa watu (anapokuwa peke yake haswali) kujionyesha sampuli hii ndio kujionyesha kuliko nyuma ya matendo. Ni shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya dini. Mpaka hapa tumebainikiwa kuwa kujionyesha kumegawanyika aina mbili:

1 – Kujionyesha ambapo ndio lengo lililo nyuma ya kitendo. Mfano wa hilo tayari limekwishalitajwa.

2 – Kujionyesha ambapo kunayasibu matendo. Ni pale ambapo mtu kwa mfano atasimama kwa lengo la kuswali kwa ajili ya Allaah. Lakini pindi atapoona mtu anamtazama wakati anaposwali anaipamba swalah yake kwa sababu ya mtu huyo. Hiki ni kitu kimeingia ndani ya kitendo. Mfano mwingine ni pale mtu anapotoa kalima au muhadhara na akaingiwa ndani ya nafsi yake kuupamba ili aweze kusifiwa na kuambiwa kuwa ni msomi au mfano wa hayo. Hiki ni kitu kimeingia ndani ya kitendo. Ni shirki ndogo. Kitu kama hichi kinaweza kupelekea kubatilishwa kwa kitendo hicho au kupunguzwa thawabu zake.

Miongoni mwa shirki ndogo ni shirki ya kunasibisha neema kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Mfano wa mtu akasema:

“Kama isingelikuwa mbwa basi tungeingiliwa na wezi.”

Badala yake anatakiwa kusema:

“Kama isingelikuwa Allaah kisha fulani basi kungelikuwa hivi na vile… “

Haijuzu kusema:

“Kama isingelikuwa fulani basi kungelikuwa hivi na vile.”

Kwa sababu msemo kama huu unapelekea katika shirki.

[1] 27:14

[2] 04:142

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 61-65
  • Imechapishwa: 07/10/2021