Haikusuniwa kwa ajili ya swalah ya ´iyd kutoa adhaana wala kukimu. Muslim amepokea kupitia kwa Jaabir ambaye ameeleza:

”Niliswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si mara moja wala mara mbili ambapo anaaza kuswali kabla ya kutoa Khutbah pasi na adhaana wala Iqaamah.”

Atasema ”Allaahu Akbar” mara sita katika Rak´ah ya kwanza baada ya Takbiyrat-ul-Ihraam na du´aa ya kufungulia swalah na kabla ya kuomba ulinzi dhidi ya shaytwaan na kabla ya kuanza kisomo al-Faatihah.  Takbiyrat-ul-Ihraam ni nguzo ambayo mtu analazimika kuileta. Swalah haifunguki pasi nayo. Takbiyr nyenginezo zimependekezwa tu. Halafu ndio atasoma du´aa ya kufungulia swalah baada  ya Takbiyrat-ul-Ihraam. Du´aa ya kufungulia swalah inakuwa mwanzoni mwa swalah. Baada ya hapo ndio ataleta Takbiyr zenye kuzidi. Halafu ndio ataomba du´aa ya kuomba ulinzi punde tu baada ya kupiga Takbiyr ya sita. Kwa sababu kuomba ulinzi kunakuwa kwa ajili ya kisomo na hivyo kunafanywa kabla ya mtu kuanza kusoma. Baada ya hapo ndio aanze kusoma al-Faatihah.

Katika Rak´ah ya pili kabla ya kuanza kusoma al-Faatihah atasema ”Allaahu Akbar” mara tano tukiondoa ile Takbiyr aliyoinuka kwayo. Ahmad amepokea kupitia kwa ´Amr bin Shu´ayb, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake aliyesimulia:

”Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alileta Takbiyr katika [swalah ya] ´iyd Takbiyr kumi na mbili;  saba katika ile [Rak´ah] ya kwanza na tano katika ile [Rak´ah] ya mwisho.”

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

Kumepokelewa mengine kuhusu idadi ya Takbiyr[1]. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wametofautiana juu ya idadi ya Takbiyr [za ´iyd]. Zote zinafaa.”

Atanyanyua mikono yake pamoja na kila Takbiyr. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akinyanyua mikono yake pamoja na  Takbiyr.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/takbiyr-za-swalah-ya-iyd-ni-jambo-lenye-wasaa/

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mulakhaswsw-ul-Fiqh (01/252)
  • Imechapishwa: 29/07/2020