Takbiyr za swalah ya ´iyd ni jambo lenye wasaa

2997- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msisahau, kama Takbiyr ya jeneza.”

Ameipokea at-Twahaawiy katika ”Sharh-ul-Ma´aaniy kupitia njia mbili kutoka kwa ´Abdullaah bin Yuusuf, kutoka kwa Yahyaa bin Hamzah: al-Wadhwiyn bin ´Atwaa´ amenihadithia kwamba al-Qaasim Abu ´Abdir-Rahmaan amemuhadithia: Baadhi ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walimuhadithia:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha siku ya ´iyd. Akapiga Takbiyr nne katika kila Rak´ah. Alipomaliza akatugeukia na kusema: ”Msisahau, kama Takbiyr ya jeneza.”

at-Twahaawiy amesema:

”Cheni ya wapokezi ni nzuri.”

Sahihi… Yanayozidi kutilia nguvu ni yale aliyopokea ´Abdur-Razzaaq kutoka kwa ath-Thawriy, kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa ´Alqamah na al-Aswad bin Yaziyd ambaye amesema:

”Ibn Mas´uud alikuwa akileta Takbiyr tisa kwenye swalah mbili za ´iyd katika kila Rak´ah; Takbiyr nne kabla ya kisomo, kisha anapiga Takbiyr na kwenda katika Rukuu´. Katika Rak´ah ya pili anaanza kusoma kwanza, anapomaliza analeta Takbiyr nne, kisha analeta Takbiyr kabla ya Rukuu´.”[1]

Cheni ya wapokezi ni Swahiyh, kama alivosema Ibn Hazm na wengineo.

Imepokelewa pia na Ibn Abiy Shaybah na al-Bayhaqiy kutoka kwa Ma´bad bin Khaalid, kutoka kwa Kardus aliyesema:

”Wakati Sa´d bin Abiy Waqqaas alipofika kabla ya ´Iyd-ul-Adhwhaa, alituma ujumbe kwa ´Abdullaah bin Mas´uud, Abu Muusa na Abu Mas´uud al-Answaariy akiwauliza idadi ya Takbiyr. Wakaliegemeza jambo la ´Abdullaah ambaye akasema: ”Ataleta Takbiyr nne, kisha atasoma na baada ya hapo atasoma Takbiyr ya tano kabla ya kwenda katika Rukuu´. Halafu atainuka, atasoma Suurah, atalete Takbiyr nne kisha na ataenda Rukuu´ katika hiyo Takbiyr ya nne.”

Cheni ya wapokezi kwenda mpaka kwa Kardus ni Swahiyh.

´Abdullaah bin al-Haarith amesema:

”Ibn ´Abbaas alituswalisha siku ya ´iyd. Akaleta Takbiyr tisa: tano katika ile ya mwanzo na nne katika ile ya pili, baada ya visomo viwili.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Bukhaariy na Muslim.

Inapokuja katika Takbiyr ya swalah mbili za ´iyd jambo ni lenye wasaa. Yule mwenye kutaka kuleta Takbiyr nne katika kila Rak´ah, basi anaweza kufanya hivo kutokana na Hadiyth na mapokezi haya. Yule anayetaka kuleta Takbiyr tano katika ya mwanzo na tano katika ya pili kutokana na Hadiyth ya al-Bayhaqiy, anaweza kufanya hivo. Ni jambo limepokelewa kutoka kwa kikosi cha Maswahabah ambazo zote kwa pamoja zinaweza kufika katika ngazi ya kuwa ni Swahiyh. Kitendo cha at-Twahaawiy kuzidhoofisha ni jambo lisilokuwa na maana yoyote, jambo ambalo linaweza kusemwa pia juu ya maoni ya wale wanaompinga pindi wanapodhoofisha dalili zake. Usawa ni kwamba yote hayo yanafaa. Yoyote utakayofanya basi umeitekeleza Sunnah. Hakuna haja ya kasumba na kuleta mfarakano, ingawa Takbiyr saba katika ile Rak´ah ya kwanza na tano katika ile ya pili ndio jambo linalopendeza zaidi kwangu, kwa sababu ndilo lililopokelewa kwa wingi zaidi.

[1] al-Muswannaf.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahâdîth as-Sahîhah (6/2/1263-1264)
  • Imechapishwa: 28/07/2020