Mtu afanye nini akiwa na mashaka juu ya maiti anayetaka kumswalia?

Swali: Imamu akiletewa kuswalia jeneza la mtu ambaye ana shaka juu ya Uislamu wake afanye nini?

Jibu: Ni wajibu kwake kumswalia. Asli ni kuwa muislamu anabaki juu ya Uislamu wake. Lakini wakati wa du´aa ashurutishe kwa kusema:

“Ee Allaah! Ikiwa ni muumini msamehe na umrehemu.” Allaah anajua kuwa ni muumini au si muumini. Akifanya hivi atakuwa amesalimika kumuombea msamaha na rehema mtu ambaye si muislamu.

Kufanya Istithnaa´ au kuweka sharti katika du´aa ni jambo limethibiti katika Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ أَزْوَاجَهُمْ وَلَمْ يَكُن لَّهُمْ شُهَدَاءُ إِلَّا أَنفُسُهُمْ فَشَهَادَةُ أَحَدِهِمْ أَرْبَعُ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ ۙ إِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ وَالْخَامِسَةُ أَنَّ لَعْنَتَ اللَّـهِ عَلَيْهِ إِن كَانَ مِنَ الْكَاذِبِينَ

“Na wale wanaowatuhumu wake zao [uzinzi] na wasiwe na mashahidi isipokuwa wao wenyewe, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa ni kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Allaah kwamba yeye ni miongoni mwa wakweli na mara ya tano [anatakiwa aape] kwamba laana ya Allaah iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.”[1]

Akasema juu ya mwanamke:

وَيَدْرَأُ عَنْهَا الْعَذَابَ أَن تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ ۙ إِنَّهُ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ وَالْخَامِسَةَ أَنَّ غَضَبَ اللَّـهِ عَلَيْهَا إِن كَانَ مِنَ الصَّادِقِينَ

“Na itamwondokea [mke] adhabu [ya kupigwa mawe], atakapotoa ushahidi mara nne kwa kiapo cha Allaah kwamba yeye [mumewe] ni miongoni mwa waongo na [atatakiwa vilevile aape kiapo] cha tano kwamba ghadhabu ya Allaah iwe juu yake ikiwa [mumewe] ni miongoni mwa wakweli.”[2]

Kufanya Istithnaa´ katika du´aa ni jambo limethibiti. Ni kama kufanya Istithnaa´ katika ´ibaadah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia binti wa Dhwibaa´ah bint az-Zubayr (Radhiya Allaahu ´anhaa) pindi alipotaka kuhiji ilihali ni mgonjwa ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amemwambia:

“Hiji na ushurutishe utasimama pale utapozuilika.”

Muhimu ni kuwa katika hali kama hii mtu afanye Istithnaa´:

“Ee Allaah! Ikiwa ni muumini msamehe.

 Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ametaja katika “I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” kutoka kwa mwalimu wake Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ya kwamba alitatizwa na masuala fulani ya kielimu ambapo akamuota Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Miongoni mwa mambo yaliyomtatiza ni kuwa aliletewa jeneza ambalo halijui kuwa ni muislamu au sio muislamu ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Ahmad! Weka sharti.”

Hivi ndivyo alivyomwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndotoni. Hii ni isnadi ya Ibn-ul-Qayyim kutoka kwa mwalimu wake Ibn Taymiyyah. Ni isnadi sahihi kwa kuwa wote wawili ni waaminifu.

Mtu asiseme kuwa sisi tumeyategemeza haya juu ya kuthibitisha hukumu ya Kishari´ah kwa maoni. Upokezi huu unatiliwa nguvu na Qur-aan, kama ilivyothibiti kwenye Suurah “an-Nuur”. Upokezi huu unaafikiana na misingi ya Kishari´ah. Hivyo ni sawa kuutendea kazi.

[1] 24:06-07

[2] 24:08-09

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/115-117)
  • Imechapishwa: 07/09/2021