Kuvaa soksi mguu wa kulia kabla ya kuosha mguu wa kushoto

Swali: Baadhi ya watu wamenambia kwamba haijuzu katikati ya wudhuu´ kuanza kuvaa soksi za mguu wa kuliani kabla ya kumaliza kuosha mguu wa kushotoni. Kipo kitabu nilichosoma muda mrefu juu ya maudhui haya na kwa sasa sikumbuki jina la kitabu hicho kinachosema kwamba kuna tofauti na maoni yenye nguvu zaidi ya wanazuoni ni kwamba inafaa.

Jibu: Bora na salama zaidi ni mtu asivae soksi mpaka kwanza amalize kuosha mguu wake wa kushoto. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapotawadha mmoja wenu na akavaa soksi zake za ngozi, basi apanguse juu yazo na aswali ndani yazo na asizivue – akitaka. Isipokuwa kutokamana na janaba.”

Ameipokea ad-Daaraqutwniy, al-Haakim ambaye ameisahihisha kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh).

Pia Abu Bakrah ath-Thaqafiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Amemruhusu msafiri kupangusa juu yake michana mitatu na nyusiku zake na mkazi mchana mmoja na usiku wake akijitwahirisha na akavaa soksi za ngozi.”

Ameipokea ad-Daaraqutwniy na ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Khuzaymah.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa al-Mughiyrah bin Shu´bah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba alimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitawadha ambapo akataka kumvua soksi zake na yeye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Ziache. Nilizivaa nikiwa katika hali ya twahara.”

Udhahiri wa Hadiyth hizi na nyenginezo zilizokuja zikiwa na maana hiyo zinafahamisha kwamba haijuzu kwa muislamu kufuta juu ya soksi isipokuwa ikiwa alizivaa baada ya kukamilika twahara. Ambaye ameingiza soksi za ngozi kwenye mguu wake wa kulia kabla ya mguu wa kushoto hajakamilisha twahara yake.

Wapo baadhi ya wanazuoni wengine wamejuzisha kupangusa ijapo mpangusaji atakuwa ameingiza soksi za ngozi kwenye mguu wake wa kulia kabla ya kuosha mguu wa kushoto kwa sababu kila soksi moja katika hizo mbili imeingizwa baada ya uoshaji.

Salama zaidi na yale maoni ya kwanza. Isitoshe ndio udhahiri wa dalili. Ambaye amefanya hivo basi anatakiwa kuvua soksi kutoka kwenye mguu wake wa kulia kabla ya kupangusa kisha arudie kuiingiza baada ya kuosha mguu wa kushoto ili atoke nje ya tofauti na afanye lililo salama zaidi juu ya dini yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/116)
  • Imechapishwa: 26/08/2021