Swali: Je, imeshurutishwa kupangusa juu ya soksi za ngozi iwe maalum au inaweza kuwa soksi ya ngozi aina nyingine yoyote?

Jibu: Ni sharti ili ifae kupangusa juu ya soksi za ngozi iwe imefunika nyayo na mafundo mawili ya miguu, ziwe safi na pasi na kujali aina ya ngozi ya mnyama midhali ni mnyama aliye msafi akiwemo ngamia, ng´ombe, kondoo na mbuzi na mfano wake. Aidha mtu awe amezivaa akiwa na twahara.

Pia inafaa kupangusa juu ya soksi za kawaida ambazo ni zile zilizosokotwa kwa ajili ya kufunika nyayo katika aina ya pamba, sufi au vyenginevyo. Soksi aina hii zina hukumu moja kama soksi za ngozi. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alifuta juu ya soksi za kawaida na juu ya viatu. Hayohayo yamethibiti kutoka kwa kikosi cha Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allaahu ´anhum).

Muda wa kupangusa ni mchana mmoja na usiku wake kwa ambaye ni mwenyeji na michana mitatu na nyusiku zake kwa ambaye ni msafiri. Muda unaanza kuhesabiwa kuanzia hadathi ya kwanza kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Hilo ni kutokana na Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa juu ya hilo. Akizivaa baada ya kukamilika twahara na hayo yanahusu twahara ndogo. Kuhusu twahara kubwa haifai akapangusa juu yake. Bali ni lazima azivue na aoshe miguu. Imethibiti kuwa Swafwaan bin ´Assaal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akituamrisha pindi tunapokuwa katika safari tusivue soksi zetu za ngozi kwa michana mitatu na nyusiku zake isipokuwa tu wakati wa janaba. Lakini wakati wa kukidhi haja kubwa, haja ndogo na wakati wa kulala.”

Ameipokea an-Nasaa´iy na at-Tirmidhiy na tamko ni lake, Ibn Khuzaymah amabye ameisahihisha. Hayo yamesemwa na Haafidhw [Ibn Hajar] katika “Buluugh-ul-Maraam”.

Twahara kubwa ni kule kujitwahirisha kutokamana na janaba, heshi na damu ya uzazi. Twahara ndogo ni kule kujitwahirisha kutokamana na hadathi ndogo kama mfano wa mkojo, kutokwa na upepo na vyenginevyo katika vichenguzi vya wudhuu´.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/111)
  • Imechapishwa: 26/08/2021