Swali: Mke wangu alienda kwenye nyumba ya jirani mmoja nikakariri kumtaliki kwa sababu ya kwenda kwake bila ya idhini yangu. Nikamwambia chukua kila chako kwenye nyumba hii na mimi ni haramu kwako. Lakini wazazi wangu wawili hawakukubaliana na mimi, wakanambia: “Wewe ndiye utatoka kwenye nyumba hii na yeye (mke wako) atakaa na sisi”. Sikutamka talaka lakini nilimwambia tu: “Mimi ni haramu kwako.” Nimewauliza baadhi ya watu wakanambia kuwa hii sio talaka na wala sina juu yangu kafara. Naomba unipe kauli ya sahihi katika maudhui hii.

Jibu: Ikiwa hali ni kama alivyosema muulizaji, hakika juu yako una kafara ya Dhwihaar kwa kauli yako: “Mimi nimeharamika kwako”. Ni kama mfano wa kusema: “Wewe ni kama mgongo wa mama yangu.” Ni juu yako kutoa kafara ya Dhwihaar ikiwa hukukusudia talaka kwa kusema kwako hivi. Ikiwa kwa hili hukukusudia talaka, basi hukumu yake ni kama ya Dhwihaar. Kutokana na kauli sahihi ya wanachuoni. Ni juu yako kutoa kafara ya Dhwihaar, nayo ni kuacha mtumwa huru ambaye ni muislamu, ikiwa hukupata utafunga miezi miwili mfululizo, ikiwa hilo ni gumu kwako na wala huwezi, utalisha masikini sitini ambao ni mafakiri. Kila mmoja utampa 1,5 kg ya tende, ngano au chakula chochote ambacho kimechozoeleka hapo unapoishi. Kila masikini mmoja utampa takriban 1,5 kg kabla ya kumgusa mke wako, kabla ya kumjamii. Huu ndio wajibu wako ikiwa hukukusudia talaka. Ama uliposema: “Wewe ni haramu kwangu” ikiwa ulikusudia talaka, hili kutokana na kauli sahihi, ni kwamba ni talaka moja itakuwa imepita ikiwa hapo mwanzo ulikuwa hujamtaliki, unaweza kumrejea kwa kusema: “Nimemrejea mke wangu, au mimi namrejea mke wangu, au namrejea mke wangu”, au maneno mfano na hayo. Kwa kushuhudisha mashahidi wawili waadilifu ya kwamba umemrejea.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.alharamain.gov.sa/index.cfm?do=cms.scholarallsubjects&schid=8177
  • Imechapishwa: 01/02/2024