´Abdullaah bin Wahb bin Muslim, Imaam na Shaykh-ul-Islaam, Abu Muhammad al-Fihriy, al-Miswriy – hafidhi.
Alizaliwa mwaka 125 kwa mujibu wa Yuunus.
Alianza kutafuta elimu wakati alipokuwa na miaka 17.
Baadhi ya aliopokea kutoka kwao ni Ibn Jurayj, Maalik, al-Layth, Ibn Lahiy´ah, ´Abdur-Rahmaan bin
Ziyaad al-Ifriyqiy na wengineo.
Alikutana na baadhi ya wanafunzi wa Maswahabah wadogowadogo na alikuwa ni chombo cha elimu na hazina ya matendo.
Ibn ´Abdil-Barr amesema katika kitabu chake ”al-´Ilm”:
”Ibn Wahb amesema: ”Nilianza kujishughulisha na ´ibaadah kabla ya kujifunza elimu. Ndipo shaytwaan akaanza kucheza na akili yangu juu ya ´Iysaa bin Maryam na ni namna gani Allaah alimuumba na kadhalika. Nikaenda kwa Shaykh mmoja na kumweleza jambo hilo akasema: ”Ee Ibn Wahb! Nikasema: ”Ndio?” Akasema: ”Tafuta elimu!” Hiyo ndio ilikuwa sababu yangu ya kutafuta elimu.”
Miongoni mwa waliohadithia kutoka kwake ni mwalimu wake al-Layth bin Sa´d, ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy, Ahmad bin Swaalih, Suhnuun bin Sa´iyd na wengineo.
Ibn Wahb amesema:
”Nilimuona ´Ubaydullaah bin ´Umar ameshakuwa kipofu na amesimamisha kufundisha Hadiyth na nilimuona Hishaam bin ´Urwah ameketi katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nikasema: ”Nitapokea elimu kutoka kwa Ibn Sam´aan kisha nende kwa Ibn Hishaam. Baada ya darsa nikasimama ili kwenda kwa Ibn Hishaam, lakini nikaambiwa kuwa amelala. Nikasema: ”Basi naenda kufanya hijah kisha nitarejea.”Niliporejea akawa amekufa.”
Ibn-ul-Qaasim amesema:
”Lau akifa Ibn ´Uyaynah, basi watu wote wataenda kwa Ibn Wahb.”
Abu Zur´ah amesema:
”Nimetazama karibu Hadiyth 30.000 za Ibn Wahb na sijui kama amepokea kitu kisichokuwa na msingi wowote. Ni mwaminifu. Nimemsikia Yahyaa bin Bukayr akisema: ”Ibn Wahb ni Faqiyh zaidi kuliko Ibn-ul-Qaasim.”
Haafidhw Ahmad bin Swaalih amesema:
”Ibn Wahb amehadithia Hadiyth 100.000. Sijamuona mtu aliye na Hadiyth nyingi kama yeye. Sisi wenyewe tumepata Hadiyth 70.000 kutoka kwake.”
Nasema: ”Ni vipi asiwe bahari ya elimu ilihali ameongezea juu ya elimu yake elimu ya Maalik, Yahyaa bin Ayyuub, ´Amr bin al-Haarith na wengineo?”
Haafidhw bin Abiy al-Junayd amesema:
“Nimemsikia Musw´ab az-Zuhriy akimtukuza Ibn Wahb na akisema: “Maswali yake kwa Maalik ni Swahiyh.”
Abu Ahmad bin ´Adiy amesema katika “al-Kaamil” yake:
”Ni katika waaminifu. Sitambui kuwa amehadithia Hadiyth ambayo ni munkari mwaminifu akihadithia kutoka kwake.”
Yahyaa bin Ma´iyn amesema:
” Mwaminifu.”
Khaalid bin Khidaas amesema:
”´Abdullaah bin Wahb alisomewa kitabu ”Ahwaal-ul-Qiyaamah” [Hali za kutisha za siku ya Qiyaamah] ambapo akaanguka na kupoteza fahamu. Baada ya hapo hakuzungumza tena mpaka masiku machache kabla ya kufa – Allaah (Ta´ala) amrehemu.”
Suhnuun amesema:
”Ibn Wahb alikuwa ameyagawanya maisha yake sehemu tatu; kuchunga mipaka ya nchi, kuwafunza watu Misri na sehemu ya mwisho katika hajj. Inasemekana kwamba alihiji hijjah 36.”
Tumefikiwa na khabari kwamba Imaam Maalik alikuwa akimwandikia:
”Kwenda kwa ´Abdullaah bin Wahb, Muftiy wa watu wa Misri… ”
Hakupatapo kufanya hivo kwa mwingine.
Abu Zayd bin Abiyl-Ghamr amesema:
“Tulikuwa tukimwita Ibn Wahb daftari la elimu.”
Abut-Twaahir bin ´Amr amesema:
“Tulikuwa tumekaa na Sufyaan ath-Thawriy wakati tulipopata khabari kwamba Ibn Wahb ameaga dunia. Ndipo Ibn ´Uyaynah akasema:
”Inna lillaahi wa inna ilayhi Raaji´uun. Waislamu wote wamepatwa na msiba.”
Yuunus bin ´Abdil-A´laa amesema:
“Walikuwa wanamtaka Ibn Wahb kumfanya Qaadhiy, akakwepa. Alifariki Sha´baan mwaka 197.”
Yuunus amesimulia kutoka kwa Ibn Wahb:
“Nimezaliwa mwaka 125, nikaanza kutafuta elimu nilipokuwa na miaka 17 na akamwalika Yuunus katika harusi yangu.”
- Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (9/223-234)
- Imechapishwa: 14/10/2020
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)