´Abdullaah bin Wahb bin Muslim, Imaam na Shaykh-ul-Islaam, Abu Muhammad al-Fihriy, al-Miswriy – hafidhi.

Alizaliwa mwaka 125 kwa mujibu wa Yuunus.

Alianza kutafuta elimu wakati alipokuwa na miaka 17.

Baadhi ya aliopokea kutoka kwao ni Ibn Jurayj, Maalik, al-Layth, Ibn Lahiy´ah, ´Abdur-Rahmaan bin
Ziyaad al-Ifriyqiy na wengineo.

Alikutana na baadhi ya wanafunzi wa Maswahabah wadogowadogo na alikuwa ni chombo cha elimu na hazina ya matendo.

Ibn ´Abdil-Barr amesema katika kitabu chake ”al-´Ilm”:

”Ibn Wahb amesema: ”Nilianza kujishughulisha na ´ibaadah kabla ya kujifunza elimu. Ndipo shaytwaan akaanza kucheza na akili yangu juu ya ´Iysaa bin Maryam na ni namna gani Allaah alimuumba na kadhalika. Nikaenda kwa Shaykh mmoja na kumweleza jambo hilo akasema: ”Ee Ibn Wahb! Nikasema: ”Ndio?” Akasema: ”Tafuta elimu!” Hiyo ndio ilikuwa sababu yangu ya kutafuta elimu.”

Miongoni mwa waliohadithia kutoka kwake ni mwalimu wake al-Layth bin Sa´d, ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy, Ahmad bin Swaalih, Suhnuun bin Sa´iyd na wengineo.

Ibn Wahb amesema:

”Nilimuona ´Ubaydullaah bin ´Umar ameshakuwa kipofu na amesimamisha kufundisha Hadiyth na nilimuona Hishaam bin ´Urwah ameketi katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nikasema: ”Nitapokea elimu kutoka kwa Ibn Sam´aan kisha nende kwa Ibn Hishaam. Baada ya darsa nikasimama ili kwenda kwa Ibn Hishaam, lakini nikaambiwa kuwa amelala.  Nikasema: ”Basi naenda kufanya hijah kisha nitarejea.”Niliporejea akawa amekufa.”

Ibn-ul-Qaasim amesema:

”Lau akifa Ibn ´Uyaynah, basi watu wote wataenda kwa Ibn Wahb.”

Abu Zur´ah amesema:

”Nimetazama karibu Hadiyth 30.000 za Ibn Wahb na sijui kama amepokea kitu kisichokuwa na msingi wowote. Ni mwaminifu. Nimemsikia Yahyaa bin Bukayr akisema: ”Ibn Wahb ni Faqiyh zaidi kuliko Ibn-ul-Qaasim.”

Haafidhw Ahmad bin Swaalih amesema:

”Ibn Wahb amehadithia Hadiyth 100.000. Sijamuona mtu aliye na Hadiyth nyingi kama yeye. Sisi wenyewe tumepata Hadiyth 70.000 kutoka kwake.”

Nasema: ”Ni vipi asiwe bahari ya elimu ilihali ameongezea juu ya elimu yake elimu ya Maalik, Yahyaa bin Ayyuub, ´Amr bin al-Haarith na wengineo?”

Haafidhw bin Abiy al-Junayd amesema:

“Nimemsikia Musw´ab az-Zuhriy akimtukuza Ibn Wahb na akisema: “Maswali yake kwa Maalik ni Swahiyh.”

Abu Ahmad bin ´Adiy amesema katika “al-Kaamil” yake:

”Ni katika waaminifu. Sitambui kuwa amehadithia Hadiyth ambayo ni munkari mwaminifu akihadithia kutoka kwake.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

” Mwaminifu.”

Khaalid bin Khidaas amesema:

”´Abdullaah bin Wahb alisomewa kitabu ”Ahwaal-ul-Qiyaamah” [Hali za kutisha za siku ya Qiyaamah] ambapo akaanguka na kupoteza fahamu. Baada ya hapo hakuzungumza tena mpaka masiku machache kabla ya kufa – Allaah (Ta´ala) amrehemu.”

Suhnuun amesema:

”Ibn Wahb alikuwa ameyagawanya maisha yake sehemu tatu; kuchunga mipaka ya nchi, kuwafunza watu Misri na sehemu ya mwisho katika hajj. Inasemekana kwamba alihiji hijjah 36.”

Tumefikiwa na khabari kwamba Imaam Maalik alikuwa akimwandikia:

”Kwenda kwa ´Abdullaah bin Wahb, Muftiy wa watu wa Misri… ”

Hakupatapo kufanya hivo kwa mwingine.

Abu Zayd bin Abiyl-Ghamr amesema:

“Tulikuwa tukimwita Ibn Wahb daftari la elimu.”

Abut-Twaahir bin ´Amr amesema:

“Tulikuwa tumekaa na Sufyaan ath-Thawriy wakati tulipopata khabari kwamba Ibn Wahb ameaga dunia. Ndipo Ibn ´Uyaynah akasema:

”Inna lillaahi wa inna ilayhi Raaji´uun. Waislamu wote wamepatwa na msiba.”

Yuunus bin ´Abdil-A´laa amesema:

“Walikuwa wanamtaka Ibn Wahb kumfanya Qaadhiy, akakwepa. Alifariki Sha´baan mwaka 197.”

Yuunus amesimulia kutoka kwa Ibn Wahb:

“Nimezaliwa mwaka 125, nikaanza kutafuta elimu nilipokuwa na miaka 17 na akamwalika Yuunus katika harusi yangu.”

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (9/223-234)
  • Imechapishwa: 14/10/2020