Ibn Baaz kuhusu ”Swifatu Swalaat-in-Nabiy” cha al-Albaaniy

Swali: Unasemaje juu ya kitabu ”Swifatu Swalaat-in-Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)” cha Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy[1]?

Jibu: Ni kitabu kizuri na chenye faida. Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy ni mtu mwanachuoni, ´Allaamah. Mwenye utukufu. Ni mtu ana jitihada kubwa katika kuzihuisha Sunnah na kupambanua kati ya ambazo ni Swahiy na dhaifu. Anatakiwa kushukuriwa kutokana na juhudi yake – Allaah amjaze kheri na amlipe maradufu.

Kila mmoja anakosea. Hakuna mwanachuoni yeyote ambaye amekingwa na kukosea. Wakati fulani inaweza kumtokea akakosea katika vitabu vyake. Hiyo ndio hali kwa wanachuoni wengine ambao ni wakubwa zaidi kuliko yeye. Wakati fulani anaweza kutokewa na makosa. Mfano wa kosa lililomtokea katika ”Swifatu Swalaat-in-Nabiy” ni pale anaposema kuwa mswaliji baada ya kuinuka kutoka kwenye Rukuu´ anatakiwa kuachilia mikono yake. Hili ni kosa. Sahihi ni kwamba anatakiwa kuirudisha juu ya kifua kama alivyokuwa amefanya kabla ya kwenda katika Rukuu´. Hili ndio jambo la sawa kutoka katika zile Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye aliweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto pindi alipokuwa anasimama na kuswali. Hili linakusanya kabla ya Rukuu´ na baada ya Rukuu´. Kadhalika Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kupitia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtu alikuwa akiamrishwa kuweka mkono wake wa kuume juu ya dhiraa yake ya kushoto ndani ya swalah.”

Ni jambo linalotambulika kwamba mswaliji huweka mikono yake kwenye magoti katika Rukuu´, huiweka ardhini katika Sujuud na katika mapaja au magoti wakati ambapo ameketi chini. Hakuna hali iliobaki isipokuwa wakati wa kusimama. Katika hali ya kusimama anatakiwa kuweka mkono wake wa kuume juu ya mkono wake wa kushoto, kifundo cha mkono na kigasha. Hiki ndio kitu ambacho anakosolewa kwacho mtunzi wa kitabu – Allaah amuwafikishe. Kama tulivyotangulia kusema kwamba kila mmoja anakosea. Mwanamme huyo ni mwenye kushukuriwa kwa kazi yake nzuri, juhudi yake nzuri na kuitilia kwake bidii Sunnah. Allaah amjaze kheri na atuzidishie sisi, nyinyi na yeye kheri na uongofu.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/category/makala/fiqh/swalah/swifatu-swalaat-in-nabiy/

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.binbaz.org.sa/mat/10506
  • Imechapishwa: 15/10/2020