Hijaab ya mwanamke mbele ya kafiri ni mkazo zaidi

Swali: Ni kiasi gani cha Hijaab kilichotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah? Je, ni kwamba mwanamke ni uchi hadi uso wake au kwamba mwanamke anawajibika kufunika uso wake wote?

Jibu: Mwanamke wote ni uchi; uso wake, mguu wake, mkono wake na kichwa chake. Vyote hivyo ni uchi. Ni wajibu juu yake kujisitiri mbele ya watu wote isipokuwa Mahram zake, ndani na nje, hata katika nchi za makafiri. Baadhi ya watu wanaona kuwa hakuna neno wakisafiri kwenda Ulaya na kwenginepo, jambo ambalo ni kosa. Kuvaa Hijaab mbele ya kafiri ni wajibu na mkazo zaidi kuliko Hijaab mbele ya muislamu. Wajibu ni Hijaab katika nchi za Uislamu na katika nchi za ukafiri. Ikiwa kunahitajika, ikiwa kwa mfano kujisitiri kunamzuia kuona, basi afanye tundu kwa jicho lake kwa kiasi cha jicho tu au macho mawili, hapo hakuna ubaya. Hivyo ndivo ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa); afanye tundu kwa kiasi cha jicho lake ili aone njia yake, asizuiwe na njia. Ikiwa anaona njia kupitia nyuma ya Hijaab, basi ni vyema. Anasema ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

”Walipokuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alisema: “Tulikuwa ikiwa wanaume wanakaribia kwetu, mmoja wetu anashusha mtandio wake juu ya uso wake. Wakiondoka mbali nasi, tunafunua.”

Kwa hiyo mwanamke akiwa peke yake au kati ya wanawake, basi anafunua. Akiwa karibu na wanaume, basi anashusha jilbaab na mtandio wake juu ya uso wake, hata kama yuko ndani ya Ihraam, mpaka wanaume waondoke mbali naye.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3489/بيان-الحجاب-الواجب-على-النساء
  • Imechapishwa: 04/09/2026