Hadiyth “Mmoja wenu asitamani mauti kwa sababu ya madhara [matatizo] yaliyompata… “

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

40 – Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

وعن أنس- رضي الله عنه- قال: قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: ((لا يتمنين أحدكم الموت لضر أصابه، فإن كان لابد فاعلاً فليقل : اللهم أحيني ما كانت الحياة خيراً لي، وتوفني إذا كانت الوفاة خيراً لي)) (متفق عليه)

“Mmoja wenu asitamani mauti kwa sababu ya madhara [matatizo] yaliyompata. Ikiwa hakuna budi isipokuwa kufanya hivo basi na aseme: “Ee Mola wangu nipe uhai ikiwa uhai una kheri na mimi na unifishe ikiwa kufa kuna kheri na mimi.” “[1]

Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu asitamani mauti kutokana na madhara yaliyompata, tusemeje juu ya yule mwenye kujiua anapofikwa na matatizo? Kuna wapumbavu wanapofikwa na matatizo wanajiua, kujilipua, kunywa sumu au mfano wa hayo. Watu hawa wameikimbia adhabu na kuiendea ambayo ni kubwa na kali zaidi kuliko waliyoikimbia. Hawatopata starehe [kwa hilo]. Wamekwepa adhabu na kuiendea nyingine ambayo ni kali zaidi. Kwa sababu yule mwenye kuiua nafsi yake ataadhibiwa kwa kile kitu alichojiua nacho ndani ya Moto wa Jahannam, atadumishwa humo milele kama ilivyokuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akijiua kwa chuma, kisu, msumari au chengenecho, siku ya Qiyaamah ndani ya Jahannam atajiua nafsi yake mwenyewe kwa chuma hichi alichotumia wakati wa kujiua.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/246-247)
  • Imechapishwa: 07/03/2023