Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

40 – Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

وعن أنس- رضي الله عنه- قال: قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: ((لا يتمنين أحدكم الموت لضر أصابه، فإن كان لابد فاعلاً فليقل: اللهم أحيني ما كانت الحياة خيراً لي، وتوفني إذا كانت الوفاة خيراً لي)) (متفق عليه)

“Mmoja wenu asitamani mauti kwa sababu ya madhara [matatizo] yaliyompata. Ikiwa hakuna budi isipokuwa kufanya hivo basi na aseme: “Ee Mola wangu nipe uhai ikiwa uhai una kheri na mimi na unifishe ikiwa kufa kuna kheri na mimi.” “[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mtu kutamani mauti kutokana na matatizo yaliyomfika. Mtu anayetamani mauti kutokana na matatizo yaliyomfika hana subira. Lililo la wajibu ni mtu anatakiwa kuwa na subira juu ya matatizo na atarajie malipo kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Hakika matatizo mbali mbali yanayomfika; hamu, machungu, magonjwa na mengineyo yanafuta madhambi madogo madogo. Endapo atataraji malipo kutoka kwa Allaah, basi ananyanyuliwa daraja.

Matatizo mbali mbali yanayomfika mtu; ikiwa ni pamoja na maudhi, maradhi na mengineyo hayadumu. Ni lazima itafika siku yataisha. Yakiisha ilihali ni mwenye kuchuma thawabu kwa kutarajia malipo kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall), basi Allaah anakusamehe kwayo madhambi. Hilo linakuwa ni kheri kwako.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/250)
  • Imechapishwa: 07/03/2023