12. Hukumu mbalimbali kuhusu Zakaat-ul-Fitwr

Mtu anatakiwa kuitoa katika ile nchi ambayo amekamilisha Ramadhaan akiwa hapo kabla ya kuswaliwa swalah ya ´iyd. Kufanya hivo ndio bora. Inafaa vilevile kuiharakisha siku moja au mbili kabla ya ´iyd. Hilo ni kutokana na kitendo cha baadhi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Abu Daawuud amesema:

“Nimemsikia Ahmad akiulizwa kuhusu kutoa Zakaat-ul-Fitwr kabla ya swalah ambapo akajibu: “Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa akiitoa siku moja au mbili kabla ya [´Iyd] al-Fitwr na yeye ndiye amepokea Hadiyth.”[1]

Ikiwa ´iyd imejulikana baada ya swalah, wakati wa kutolewa kwake kumemkuta mtu akiwa nje ya nchi au yuko katika nchi ambayo hakuna wenye kuistahiki, basi itasihi kuitoa baada ya swalah.

Haijuzu kutoa pesa badala ya chakula kwa mujibu wa moja kati ya maoni mawili. Kwa sababu linaenda kinyume na dalili. Abu Daawuud amesema:

“Ahmad aliulizwa na mimi nikisikia: “Atoe pesa?” Akajibu: “Nachelea isisihi kwa sababu ni jambo linaenda kinyume na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Mtu ajitolee mwenyewe na wale ambao analazimika kuwahudumia kama vile mke na watoto wake wasipoweza kujitolea wenyewe. Wakiweza basi watajitolea wenyewe. Kwa sababu wao ndio wanaozungumzishwa kwayo, kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) iliotangulia.

Inapendeza pia kumtolea mtoto aliye tumboni akishakamilisha miezi minne[3].

Ni lazima kwa mtu ahakikishe wanaipokea watu wanaostahiki. Wako watu ambao wamezowea kujitolea zakaah zao na zakaah za familia zao kuwapa watu maalum kwa ajili ya malengo fulani, kitendo ambacho hakifai. Zakaah ni haki ya Allaah (Ta´ala) ambayo haijuzu kufanya upendeleo kwayo. Pengine hali ya mtu huyo imekwishabadilika na hivyo akawa si mwenye kustahiki.

Inafaa kwa fakiri akipokea zakaah kutoka kwa mtu akajitolea nayo mwenyewe au mmoja katika familia yake ikithibitishwa na wakala wake.

Haijuzu kwa mtu kutoa vitu vibaya katika zakaah. Allaah ni mzuri na hakubali isipokuwa vilivyo vizuri. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ ۖ وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلَّا أَن تُغْمِضُوا فِيهِ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ

 “Enyi mlioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambayo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa na hali nyinyi wenyewe si wenye kuvichukuwa isipokuwa kwa kuvifumbia macho. Na tambueni kuwa hakika Allaah ni Mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.” (02:267)

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] Masaa-il al-Imaam Ahmad (85)

[2] Masaa-il al-Imaam Ahmad (85) na tazama “al-Mughniy” (04/295).

[3] al-Mahallaa (06/132), ”Sharh-ul-Mumtaa´” (06/161).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 79
  • Imechapishwa: 07/03/2023