8 – ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaradhisha kutoa pishi ya tende au pishi ya shayiri kuwa ni Zakaat-ul-Fitwr iliyowajibika kwa waislamu wote; mtumwa na aliye huru, mwanamume, mwanamke, mtoto mdogo na mzee na kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha ulazima wa kutoa Zakaat-ul-Fitwr kwa mkubwa na mdogo, mwanamme na mwanamke, muungwana na mtumwa katika waislamu. Lengo ni kumsafisha mfungaji kutokana na yale mambo yanayochafua funga yake na kupunguza thawabu zake. Jengine ni kuwalisha wafungaji katika siku ya furaha na kufurahika. Ndani yake kuna kusifika na ukarimu na usawa. Ndani yake mtu anadhihirisha kushukuru neema ya Allaah kwa kukamilisha swawm na kusimama usiku na pia kufanya yale ayawezayo katika matendo mema.

Kiwango cha Zakaat-ul-Fitwr ni pishi ya chakula kama vile ngano, shayiri, tende, zabibu, maziwa ya unga au chakula kingine kinacholiwa katika mji kinachosimama mahali pake kama vile mchele. Kiwango cha pishi ni 2,4 kg.

[1] al-Bukhaariy (1503) na Muslim (984).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 78-79
  • Imechapishwa: 07/03/2023