Tawbah ya kweli iliyoamrishwa na Allaah ina sharti tano. Nazo ni kama ifuatavyo:

1 – Ikhlaasw. Tawbah yake iwe takasifu kwa ajili ya Allaah. Atubie dhambi kwa ajili ya kumtii Allaah (´Azza wa Jall), kumpenda, kumtukuza, kutaraji thawabu na kuogopa adhabu Yake.

2 – Aache maasi aliyokuwa akiyafanya. Ikiwa ni jambo la haramu basi aliache papohapo. Ikiwa ni kuacha jambo la wajibu na anaweza kulilipa, basi aharakishe kulitekeleza kama mfano wa zakaah. Ikiwa ni maasi yanayohusiana na haki ya mtu, kama vile mali, basi amrudishie mwenye nayo akiwa hai, au warithi wake akiwa ameshakufa. Akiwa hamjui mwenye nayo basi amtolee nayo swadaqah. Ikiwa haki ni usengenyi – ikiwa msengenywa anajua kuwa alisengenywa au anaogopa kumjuza – vinginevyo amuombe msamaha. Badala ya usengenyi amsifu katika kikao kilekile ambacho alimsengenya. Kwani hakika mema yanafuta maovu.

3 – Miongoni mwa sharti za tawbah ni ajutie kufanya maasi na atamani lau asingeyafanya ili hayo yamfanye kuwa mnyonge na kujivunjavunja mbele ya Allaah (Ta´ala).

4 – Aazimie kutorudi maishani. Haya ndio matunda ya tawbah. Isitoshe ni alama ya kuonyesha ukweli wa tawbah yake.

5 – Tawbah iwe ndani ya wakati wake uliopangwa. Ikifanywa nje ya wakati wake haitokubaliwa. Yamethibitisha hilo yale aliyopokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutubu kabla ya jua kuchomoza upande wa magharibi basi Allaah atamsamehe.”[1]

´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hukubali tawbah ya mja muda wa kuwa hajakuwa katika hali ya kukata roho.”[2]

Bi maana muda wa kuwa roho yake haijafika kooni. Katika hali hiyo inakuwa ni kama kitu ambacho kinamfanya mgonjwa kugunaguna.

[1] Muslim (2703).

[2] at-Tirmidhiy (3537), Ibn Maajah (4253) na Ahmad (10/300).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 07/03/2023