07 – al-Agharr bin Yasaar al-Muzaniy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi watu! Tubuni kwa Allaah. Kwani hakika mimi natubia Kwake mara mia kwa siku.”[1]

Ameipokea Muslim.

Hadiyth inajulisha ulazima wa kila mtu kutubia. Hii ni amri ambayo inapelekea katika uwajibu. Amesema (Ta´ala):

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, ili mpate kufaulu.”[2]

وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ

”Na kwamba mwombeni Mola wenu msamaha kisha tubuni Kwake.”[3]

Ni lazima kwa kila mja kutubia. Mtu hakusalimika na madhambi au mapungufu katika kumtii Allaah (Ta´ala). Kama ambavo tawbah inafanywa wakati wa kutenda makosa inafanywa vilevile wakati wa kuacha mema yaliyoamrishwa. Tawbah ni lazima papohapo. Haijuzu kuichelewesha. Mtu hajui ni lini kifo kitamjilia. Jengine ni kwa sababau matendo maovu huvuta mengine. Hapo ni pale ambapo mtu anayaendeleza maasi, jambo ambalo linapelekea katika ususuwavu wa moyo na kuwa mbali na Allaah (Ta´ala). Aidha jambo hilo linapelekea kudhoofika kwa imani. Kwa sababu imani inazidi kwa utiifu na inashuka kwa maasi.

Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu kuimaliza Ramadhaan kwa kutubia kwa Allaah na kurejea Kwake. Afanye yale yanayopendwa na Mola Wake na ajiepushe na yale yasiyomfurahisha. Vilevile aharakie kuyafanya yale yaliyompita mwanzoni mwa mwezi katika kipindi kilichosalia cha mwezi wake na asimame mbele ya Muumba wake kisimamo cha mja dhalili, aliye na khofu na mwenye kujivunjavunja.

[1] Muslim (2702) na (42).

[2] 24:31

[3] 11:03

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 07/03/2023