08. Baadhi ya sifa za Moto na wakazi wake

06 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Moto wenu huu ambao anauwasha mwanadamu ni sehemu moja katika sehemu sabini katika joto la Jahannam.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tunaapa kwa Allaah kwamba ungelikuwa ni huu peke yake ungelitosha.” Akasema: “Hakika umependelewa kwa sehemu sitini na tisa ambazo zote ni kama moto wake.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha ukali wa Moto wa Jahannam na kwamba moto wa ulimwenguni – pamoja na joto lake kali – ni sehemu kidogo tu linalotokana na joto kali la Moto wa Jahannam. Amesema (Ta´ala):

وَأَصْحَابُ الشِّمَالِ مَا أَصْحَابُ الشِّمَالِ فِي سَمُومٍ وَحَمِيمٍ وَظِلٍّ مِّن يَحْمُومٍ  لَّا بَارِدٍ وَلَا كَرِيمٍ

”Na watu wa kushotoni – je, ni kina nani watu wa kushotoni? Watakuwa kwenye Moto ubabuao na maji yanayochemka na kivuli cha moshi mweusi mnene wa joto kali mno. Si cha kuburudisha wala kustarehesha.”[2]

´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeutazama Moto na kuona wakazi wake wengi ni wanawake.”[3]

Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amejiwabishia ahadi kwa anayekunywa kileo basi atamnywesha katika Twiynat-ul-Khabaal.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nini Twiynat-ul-Khabaal?” Akasema: “Ni jasho la watu wa Motoni” au “Usaha wa watu wa Motoni.”[4]

Allaah ametutahadharisha ndani ya Qur-aan kutokana na Moto na akatueleza aina mbalimbali ya adhabu Zake kwa ajili ya kutuonea huruma ili khofu na tahadhari yetu iweze kuongezeka. Lengo lingine ni ili tuweze kujiepusha na zile zote ambazo ni miongoni mwa sifa za watu wake.

Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu kujiepusha na Moto ambao ni makazi ya dhiki na maangamizo, makazi ya khasara na adhabu kali. Hayo yanafanyika kwa kumtii Allaah (Ta´ala) kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Aidha ajiepushe na sifa za watu wa Motoni na wakazi wake kukiwemo kumshirikisha Allaah, ukafiri, kuwakadhibisha Mitume, kuzichezea shere Aayah za Allaah, kuua, kula ribaa, kucheza na swalah, kuzuia zakaah na kuacha kufunga Ramadhaan kwa makusudi. Vilevile anatakiwa kujiepusha kutokana na maadili mabaya kukiwemo kusema uwongo, usaliti, dhuluma, utovu wa nidhamu kwa wazazi wawili, kukata udugu na mengineyo yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah.

Hadiyth hii tuliyoitaja punde inafahamisha kuwa moto tulionao duniani unatakiwa utukumbushe Moto uliopo Aakhirah. Kama alivosema (Ta´ala):

نَحْنُ جَعَلْنَاهَا تَذْكِرَةً وَمَتَاعًا لِّلْمُقْوِينَ

“Sisi tumeufanya kuwa ni ukumbusho na manufaa kwa wasafiri.”[5]

Bi maana wasafiri. Maoni mengine yanasema wanaostarehe ni mamoja mkazi au msafiri. Kwani hakuna chakula kinachopikwa bila ya moto[6]. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] al-Bukhaariy (3265) na Muslim (28463).

[2] 56:41-44

[3] al-Bukhaariy (6546).

[4] Muslim (2002).

[5] 56:73

[6] Tazama ”Tafsiyr Ibn Kathiyr” (08/19).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 73-74
  • Imechapishwa: 06/03/2023