Hadiyth “Yule ambaye Allaah anamtakia kheri, basi humpa msiba… “

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

وعن أبي هريرة- رضي الله عنه- قال: قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: ((من يرد الله به خيراً يصب منه)) (رواه البخاري)

39 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri, basi humpa msiba.”[1]

Makusudio ni kwamba yule ambaye Allaah anamtakia kheri humpa msiba na akavumilia juu ya msiba huu, basi hilo huwa ni kheri kwake. Kwa sababu tumetangulia kusema ya kwamba msiba unakuwa ni kafara ya Allaah kusamehe madhambi madogo madogo kutokana na msiba huo. Ni jambo lenye kujulikana ya kwamba kusamehewa kwa madhambi na maasi ni jambo lenye kheri kwa mtu. Hili ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote. Matatizo kiasi na yatakavyokuwa bado ni ya kidunia na hivyo ipo siku moja yataondoka. Kila jinsi siku zinavyokwenda unawepesishiwa msiba lakini adhabu ya Aakhirah bado ni yenye kubaki palepale. Hivyo Allaah akikusamehe madhambi yako kwa sababu ya msiba huu, hilo linakuwa ni kheri kwako.

[1] al-Bukhaariy

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/245)
  • Imechapishwa: 06/03/2023