Hadiyth “Allaah anapompendelea mja wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani… “

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

وعن أنس ـ رضي الله عنه ـ قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إذا أراد الله بعبده خيرا عجل له العقوبة في الدنيا، وإذا أراد بعبده الشر أمسك عنه بذنبه حتى يوافي به يوم القيامة))

43 – Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume  wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapompendelea mja wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani, na akimtakia mja wake shari humzuilia dhambi zake ili amuadhibiwa kwazo siku ya Qiyaamah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika malipo makubwa yanakuwa pamoja na mabalaa makubwa. Allaah (Ta´ala) anapowapenda watu, huwapa majaribio; yule anayeridhia basi hupata radhi [za Allaah], na yule mwenye kuchukia hupata khasira [za Allaah].”

Hadiyth ni nzuri

Mtu hakusalimika na makosa, madhambi na mapungufu katika mambo ambayo ni ya wajibu. Allaah akimpendelea mja Wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani. Ima humuadhibu katika mali yake, familia yake, yeye mwenyewe au mmoja katika watu aliyofungamana nao. Adhabu zinafuta madhambi. Allaah akimharakishia adhabu na kwa dhambi hiyo akamsamehe mja, basi Allaah humfisha ilihali hana dhambi. Matatizo na mitihani imemsafisha mpaka. Sivyo tu bali mtu kifo chake hufanywa kikawa kigumu kutokana na chembe chembe za maasi yaliyobakia ili aweze kutoka duniani ilihali amesafishwa na madhambi. Hii ni neema. Adhabu ya duniani ni nyepesi kuliko ya Aakhirah.

Upande mwingine Allaah akimtakia mja Wake shari humtunukia na kumruzuku neema na kumzuilia machungu mpaka akaingiwa na jeuri – tunaomba ulinzi kwa Allaah – na huku anafurahi furaha yenye kulaumiwa kutokana na yale Allaah aliyomneemesha. Ghafla anakutana na Allaah ilihali madhambi yamemjaa. Hatimae anaadhibiwa kwayo Aakhirah.

Ukimuona mtu amezama katika kumuasi Allaah na wakati huo huo Allaah amemtunukia neema mbali mbali na kumzuilia na matatizo, basi utambue kuwa Allaah anamtakia shari. Allaah amemcheleweshea adhabu ili aweze kupewa nayo siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/258-259)
  • Imechapishwa: 08/03/2023