Chunga ni wakati gani unauliza swali

Miongoni mwa adabu ambazo muulizaji anatakiwa kuzichunga ni kwamba afanye adabu kwa wanazuoni na wanazuoni wawe na haiba na heshima kifuani mwake. Ukiwa na heshima ya ziada kwa mwanachuoni na akahisi hilo kutoka kwako, basi atakuzidishia elimu na jawabu. Kwa sababu umehakikisha ziada. Bi maana umekuwa ni mwenye kustahiki kuzidishiwa. Kwa sababu dalili ya kwamba mwanafunzi anastahiki kufafanuliwa zaidi jibu na faida kamili kutoka kwa mwanachuoni, ni yeye afanye adabu kwake. Kwa mfano asije na kuleta baadhi ya maneno yasiyokuwa mazuri au maneno yenye ususuwavu. Bali afanye adabu na achunge wakati unaofaa kwa mwanachuoni ndio amuulize. Nyakati za mwanachuoni zinatofautiana. Kuna wakati ambao ni wa sawa kwako na si sawa kwake. Matokeo yake jibu analokupa likawa linatokana kutegemea na hali alionayo. Anaweza kuwa mwenye haraka, anaweza kuwa nyuma yake yuko na kitu, pengine umekaribia wakati wa swalah na hivyo anataka kujiandaa kutawadha na mfano wake, pengine ni wakati wa yeye kutaka kulala, pengine kuna kitu kinachomshughulisha, pengine nyumbani kuna kitu kimemshughulisha, pengine kichwani mwake kuna masuala fulani miongoni mwa masuala yaliyoko katika jamii na kadhalika. Kwa hivyo unatakiwa kuchunga wakati wa mwanachuoni wakati unapomuuliza na muulize kama ni wakati wa sawa kumuuliza au unaweza kurudi wakati mwingine. Akikwambia urudi wakati mwingine inakuwa umeonyesha heshima ya zaida, unapata thawabu kwa sababu umechunga jambo hilo na kufanya adabu. Ukija wakati mwingine kumuuliza anakuwa tayari kukujibu kwa ufafanuzi zaidi vile inavyopasa.

Siku zote anayepiga simu ndiye anakuwa katika hali nzuri. Kuhusu anayepigiwa simu haijulikani yuko na hali gani. Mpigaji simu anataraji kutoka kwa mwanachuoni amwambie kadhaa na kadhaa, amkaribishe na ampambanulie ilihali hajui hali ya anayempigia simu. Hali za watu majumbani mwao na katika makazi yao zinatofautiana. Huenda akili yake kipindi hicho ni yenye kushughulika na kadhalika. Kwa hivyo inatakiwa kuchunga jambo hilo na mtu asifikiri kuwa siku zote mwanachuoni au mwanafunzi akili yake inakuwa katika hali moja na daima anakuwa tayari kujibu jawabu lenye upambanuzi kwa dalili zake.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ‘Abdil-‘Aziyz Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muhadhara: Adab-us-Suwaal https://saleh.af.org.sa/sites/default/files/2017-11/006.mp3
  • Imechapishwa: 12/01/2023