Ndani ya gari hakuna maswali

Kwa ajili ya kuchunga adabu na kuitakasa dhimma ni lazima kutofautisha hali za kuuliza. Kuuliza msikitini baada ya muhadhara kuna hali yake, kuuliza baada ya imamu kumaliza kuswalisha kuna hali yake, kuuliza baada ya darsa ya kielimu katika Fiqh, Tawhiyd au darsa nyinginezo kuna hali yake katika namna ya kujibu na kufafanua, kuuliza kwenye simu lina hali yake, kuuliza kwenye gari kuna hali yake na hali nyenginezo.

Baadhi ya watuwazima walinieleza kwamba kuna mzee mmoja siku moja alitaka kumuuliza Shaykh Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaah) swali ndani ya gari. Shaykh akajibu kwa kusema kuwa ndani ya gari hakuna fataawaa. Tutapofika nyumbani na kuingia ndani utauliza au tutapokuwa msikitini tutaingia na utaniuliza. Kwa nini? Kwa sababu amepanda naye kwenye gari na kuna harakati nyingi zinazoendelea kuliani na kushotoni, mwenye kujibu ananukuu yale yaliyosemwa na Allaah. Mwenye kujibu anaweka saini kwa niaba ya Mola wa walimwengu. Anapokujibu ni kana kwamba anakwambia hii ndio fatwa ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) juu ya swali lako:

يَسْتَفْتُونَكَ قُلِ اللَّـهُ يُفْتِيكُمْ

“Wanakuuliza hukumu ya kishari’ah. Sema: “Allaah anakubainishieni.”” (04:176)

Haya ndio maneno ya Allaah na ndio hukumu kwa mujibu wa Shari´ah. Ni jambo kubwa. Kwa ajili hiyo Salaf wengi walikuwa wanaogopa maswali, wakawarudisha nyuma waulizaji na mara nyingi wakisema kuwa hawajui. Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) alikuwa anapoulizwa anasema kuwa hajui ilihali yeye ndiye Abu ´Abdillaah Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah). Alimjilia muulizaji kutoka nchi ya mbali na akamwambia: “Ee Abu ´Abdillaah! Nimekujia kutoka nchi fulani kutoka kwa wana na ndugu zako wanaokupenda. Wamenibebesha kazi ya kukuuliza maswali arobaini ambapo Maalik akamwambia aulize. Akauliza swali la kwanza ambapo akasema kuwa hajui, vivyo hivyo swali la pili na swali la tatu. Akajibu maswali saba na imesemekana vilevile alijibu maswali manne na maswali thelathini na tatu au maswali thelathini na sita akasema kuwa hajui. Mwanachuoni hii leo anapowaambia baadhi ya waulizaji au baadhi ya wanafunzi “sijui” wanaona kuwa hana elimu. Wakati mwingine hali inakuwa si nzuri, pengine anataka kumtia adabu muulizaji na kadhalika.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ‘Abdil-‘Aziyz Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muhadhara: Adab-us-Suwaal https://saleh.af.org.sa/sites/default/files/2017-11/006.mp3
  • Imechapishwa: 12/01/2023