Abu Daawuud amesema:

”Nilimsikia Ahmad akiulizwa kuhusu mtu anayemvisha kijakazi wake kofia. Akajibu: ”Asimvishe mavazi ya kiume. Asimfananishe na wanamme.”

Abu Daawuud amesema:

”Nilisema kumwambia Ahmad: ”Amvishe ndala?”Akajibu: ”Hapana, isipokuwa ikiwa anazivaa kwa sababu anataka kutawadha.” Nikasema: ”Kwa ajili ya kujipamba?” Akajibu: ”Hapana.” Nikamuuliza: ”Je, inafaa akamnyoa nywele zake?” Akajibu: ”Hapana.”[1]

adh-Dhahabiy ametaja mada hii katika kitabu chake ”al-Kabaair”, akataja Hadiyth zilizotangulia kisha akasema:

”Mwanamke akivaa nguo za wanamme kama vile burnus, koti na nguo za mikono yenye kubana amejifananisha na wanamme kwenye mavazi yao na hivyo amepata laana ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hilo linamgusa pia mume wake akimwacha kufanya hivo au akaliridhia na asimkataze. Kwa sababu mume ameamrishwa kumnyoosha mwanamke kumtii Allaah na kumkataza kumuasi. Amesema (Ta´ala):

قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

”Jikingeni nafsi zenu na familia zenu na Moto ambao mafutayake ni watu na mawe.”[2]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nyote ni wachungaji na kila mmoja ataulizwa kwa kile alichokichunga. Kiongozi ni mchungaji na ataulizwa kwa kile alichokichunga. Mwanaume ni mchungaji wa familia yake na yeye ataulizwa kwa kile alichokichunga. Mwanamke ni mchungaji na yeye ataulizwa juu ya nyumba ya mume wake.”[3]

[1] Masaa-il-ul-Imaam Ahmad, uk. 261. Kumekuja makatazo ya waziwazi juu ya hilo. ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mwanamke kunyoa kichwa chake.”

Ameipokea an-Nasaa’iy (2/276) na at-Tirmidhiy (2/19). Cheni yake ya wapokezi ingelikuwa Swahiyh endapo msimuliaji asingetatizika kati ya kuisimulia na kukosekana Swahabah katika cheni ya wapokezi. Licha ya kwamba anachukulia wepesi katika kusahihisha, at-Tirmidhiy ameikosoa cheni yake ya wapokezi kutokana na sababu hiyo. Nimeongelea vyanzo na njia zake zote katika ”adh-Dhwa´iyfah” (678).

Kinachodhihiri ni kwamba anachokusudia Ahmad ni uharamu wa kunyoa nywele, na si kwamba asizikate. Kwa sababu inafaa kwake kuzikata. Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan amesema:

”Mimi na kaka yake na ´Aaishah wa kunyonya tuliingia kwake. Nikamuuliza kuhusu josho ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na janaba… Wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakikata nywele zao zikafika mpaka masikioni.” (Muslim (1/176))

Inafaa kwa mwanamke kupunguza nywele zake kwa sharti isiwe kwa lengo la kujifananisha na wanawake wa kikafiri; katika hali hiyo haijuzu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”

[2] 66:6

[3] al-Bukhaariy (7138) na Muslim (1829).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 147-148
  • Imechapishwa: 18/10/2023