87. Kwenda kinyume na maumbile yaliyowekwa

al-Haytamiy ameliafiki na akasema:

”Kutokana na Hadiyth hizi Swahiyh na nyenginezo zenye matishio ni jambo la wazi kabisa kwamba matendo yaliyotajwa ni katika madhambi makubwa. Nilichofikia ni kwamba maimamu wetu wana mitazamo miwili juu ya kujifananisha huku. Maoni ya kwanza ni kwamba ni haramu. Maoni hayo yamechaguliwa na an-Nawawiy. Maoni mengine yanasema kuwa inachukiza. Maoni hayo yamechaguliwa na ar-Raafi´iy. Maoni sahihi na ya sawa ni yale aliyosema an-Nawawiy kwamba ni haramu na kutokana na zile Hadiyth zilizotangulia. Isitoshe nimewaona baadhi ya waandishi wakiingiza dhambi hiyo miongoni mwa yale madhambi makubwa.”[1]

Haafidhw Ibn Hajar amesema:

”at-Twabariy amesema: ”Haijuzu kwa mwanaume kujifananisha na mwanamke inapokuja katika mavazi na mapambo ambayo ni maalum kwa wanawake, na kinyume chake. Shaykh Abu Muhammad bin Abiy Jamrah amesema: ”Udhahiri ni kwamba makaripio ni yenye kuenea katika aina zote za kujifananisha, lakini kutokana na Hadiyth nyenginezo mtu anafahamu kuwa kilichomaanishwa ni kujifananisha katika mavazi na baadhi ya sifa, mienendo na mfano wake. Makatazo hayahusu matendo mema yanayofanywa na wanawake. Hekima ya kulaaniwa yule anayejifananisha maana yake ni kwenda kinyume na yale maumbile aliyoyaweka Mwingi wa wenye hekima. Hukumu hiyohiyo imeashiriwa wakati walipolaaniwa wanawake wanaoonganisha nywele zao pale aliposema: ”… wanawake wanaobadilisha maumbile ya Allaah kwa ajili ya kutafuta urembo.”[2][3]

Kwa maana nyingine imethibiti kuwa haijuzu mavazi ya mwanamke kufanana na mavazi ya mwanaume. Haijuzu kwa mwanamke kuvaa shuka ya chini na shuka ya juu ya mwanaume ya kuhijia na mfano wake. Baadhi ya wanawake hii leo wanavaa majaketi na suruwali. Haijuzu kwao licha ya kuwa yanawafunika vyema zaidi kuliko mavazi yao mengine ya kigeni. Zingatieni, enyi wenye kuona!

[1] az-Zawaajir (1/126).

[2] al-Bukhaariy (10/306), Muslim (6/166-167) na wengineo kupitia kwa Ibn Mas´uud, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Allaah amemlaani mwenye kufanya chanjo na mwenye kufanywa chanjo, mwenye kuunganisha nywele na mwenye kuunganishwa nywele, mwenye kuondosha nywele usoni na mwenye kuondoshwa nywele usoni –  wanawake wanaobadilisha maumbile ya Allaah kwa ajili ya kutafuta urembo.”

Azingatie yule anayebadilisha maumbile ya Allaah pasi na idhini kutoka Kwake, basi si vyenginevyo ni kwamba anamfuata shaytwaan aliyesema:

وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا

”Basi watakata masikio ya wanyama na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah. Na yule atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki badala ya Allaah, basi hakika amekhasirika khasara ya wazi kabisa.”” (4:119)

[3] Fath-ul-Baariy (10/273-274).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 149-150
  • Imechapishwa: 18/10/2023