Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

71 – Uombezi ambao amewawekea ni haki, kama ilivyopokelewa katika Hadiyth nyingi.

MAELEZO

Uombezi ni miongoni mwa mambo yanayohusu ´Aqiydah. Wako watu ambao wamepotea katika kuuthibitisha, wengine wakachupa mipaka katika kuuthibitisha na wengine wakashika msimamo wa kati na kati. Kwa maana nyingine watu wamegawanyika mafungu matatu inapokuja katika Uombezi siku ya Qiyaamah:

1 – Wako ambao wamechupa mipaka katika kuthibitisha uombezi mpaka wakafikia kuomba uombezi kutoka kwa wafu, makaburi, masanamu, miti na mawe:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao [hawawezi] kuwadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.””[1]

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٌٰ

“Na wale wanaowafanya wengine badala Yake kuwa walinzi [wakisema]: “Hatuwaabudu isipokuwa kwa lengo la kutukurubisha kwa Allaah ukaribu.”[2]

2 – Wako wengine wamepindukia mipaka katika kupinga Uombezi kama vile Mu´tazilah na Khawaarij. Wanaona kuwa waislamu watenda madhambi makubwa hawatoombewa msamaha. Hivyo wakaenda kinyume na dalili nyingi zilizopokelewa ndani ya Qur-aan na Sunnah zinazothibitisha Uombezi.

3 – Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wana msimamo wa kati na kati juu ya Uombezi. Wamethibitisha Uombezi kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah na wakaiamini bila kuchupa mipaka wala kuzembea.

[1] 10:18

[2] 39:3

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 24/01/2023