Inatakikana kwa mtu amkumbushe mgonjwa kutubu. Hata hivyo asimwambie kwa njia ya moja kwa moja kwa sababu pengine hilo likamtia woga na akasema ndani ya moyo wake lau asingeliona kuwa maradhi yangu ni khatari asingelinikumbusha kutubu. Anachotakiwa kufanya asome Aayah au Hadiyth ambazo ndani yake kuna kuwasifu wenye kutubu jambo ambalo litamfanya mgonjwa awaidhike.

Aidha anatakikana amkumbushe wasia. Asimwambie usia kwa kuwa wakati wako umekaribia. Akimwambia hivo anamtia woga. Kwa mfano anaweza kumuwaidhisha kwa kisa kilichothibiti. Kwa mfano anaweza kumwambia kuwa fulani alikuwa na deni na alikuwa ni mtu mwenye maazimio na akawausia familia yake wamlipie deni lake na mfano wa hivo katika maneno ambayo hayatomtia woga.

Wanachuoni wamesema pia ya kwamba ikiwa anaona kuwa mgonjwa anataka kusomewa basi amsomee. Anatakiwa amsomee kwa yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)…

Vilevile ukiona kuwa mgonjwa anapenda ukae kwake kwa muda mrefu basi fanya hivo. Wewe uko katika kheri na ujira. Kaa kwa muda mrefu na umfanye aweza kufurahi. Pengine kule kumfurahisha ikawa ni sababu ya kupona kwake. Kwa sababu kufurahi kwa mgonjwa na moyo wake kukunjuka ni miongoni mwa sababu kubwa za kupona kwake. Hivyo basi, ukiona kuwa anapenda uendelee kubaki basi fanya hivo na ukae kwa muda mrefu mpaka pale utapoona kuwa amechoshwa sasa. Ama ukiona kuwa mgonjwa unamtia uzito na hapendi ubaki, anapenda uende ili mke wake aweze kuja, basi usichelewe. Muulize hali yake kisha ondoka zako.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/49-51)
  • Imechapishwa: 24/01/2023