Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza pia kwamba kuna watu ambao wataenda na kufukuzwa na kuzuiwa kunywa humo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme:

“Maswahabah wangu! Maswahabah wangu!” Ndipo aambiwe: “Hakika wewe hujui yale waliyoyazua baada yako.” Aseme (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Watokee mbali wale waliobadilisha na kugeuza.”[1]

Watazuiwa na kuifikia hodhi Ahl-ul-Bid´ah wapotofu wanaoenda kinyume na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); waliokufuru, kuritadi, wenye kuiacha Sunnah na wakaenda katika matamanio na maoni yao yaliyopinda. Hawa watazuiwa kutokamana na hodhi yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa sababu wamebadilisha na kugeuza uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna wataofikia na kunywa isipokuwa tu wale waliokuwa wakifuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kimaneno, kimatendo na kiimani.

Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa hodhi ni ile Kawthar iliyotajwa katika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ

“Hakika Sisi tumekupa [mto wa] al-Kawthar!”[2]

Wengine wanaona kuwa neno (الْكَوْثَر) ni kheri nyingi. Hapana shaka kwamba hodhi inaingia ndani ya kheri hii nyingi kwa sababu ni kheri juu ya ummah huu. Ni lazima kuamini hodhi. Ni lazima vilevile mtu kushikamana barabara na Sunnah ili aweze kunywa katika hodhi hii na asifukuzwe hiyo siku ya Qiyaamah.

[1] al-Bukhaariy (6582) na Muslim (2304).

[2] 108:1

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 24/01/2023