Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

70 – Hodhi ambayo Allaah (Ta´ala) atamkirimu ili iwe ni burudisho la kiu ya ummah wake ni haki.

MAELEZO

Miongoni mwa mambo ambayo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanayaamini ni yale ambayo yamesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mambo yatayotokea siku ya Qiyaamah. Moja katika mambo hayo ni hodhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukhabarisha kuwa yuko na hodhi katika uwanja wa mkusanyiko siku ya Qiyaamah. Wataiendea wafuasi wake ambao walimuamini na kumfuata. Watakunywa humo na baada ya kunywa kamwe hawatohisi tena kiu baada yake. Qiyaamah ni siku nzito na yenye joto kali. Kiu kitakuwa kikali. Kwa ajili hiyo Allaah akafanya kuwepo kwa hodhi hii ili ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) uweze kunywa na kunyweshelezwa kwayo. Kama ambavyo Allaah huteremsha mvua ambayo ikahuisha ardhi na watu, basi vivyo hivyo Allaah kwa hodhi hiyo atawahuisha waja pindi watapokuwa ni wahitaji zaidi wa maji.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa ni hodhi kubwa. Urefu wake ni masafa ya mwezi na upana wake ni masafa ya mwezi. Vikombe vyake ni sawa na nyota mbinguni. Ambaye atakunywa humo mara moja basi kamwe hatohisi tena kiu. Maji yake ni meupe zaidi kuliko maziwa na matamu zaidi kuliko asali.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 24/01/2023